Feb 02, 2024 07:49 UTC
  • Ansarullah: US kuiasa China iingilie kadhia ya Bahari Nyekundu ni ishara ya kufeli

Kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen amesema juhudi za Washington za kutafuta usaidizi na upatanishi wa China ili iwaombe Wayemen wasimamishe mashambulizi dhidi ya meli za Marekani na Uingereza zinazopita Bahari Nyekundu zinaonesha namna madola hayo mawili ya kibeberu yalivyofeli katika mipango yao.

Abdul-Malik al-Houthi alisema hayo jana Alkhamisi katika hotuba kwa njia ya televisheni kutoka Sana'a na kuongeza kuwa, hakuna shaka kuwa China inafahamu vyema sera za kiuadui za US dhidi yake ikiwemo chokochoko za Washingtn katika eneo la Taiwan, na kwa msingi huo Beijing haiwezi kujihusisha na suala lolote la kuhudumia au kulinda maslahi ya US.

Al-Houthi ameeleza bayana kuwa, Washington na London zinapasa kubeba dhima ya kuvuruga hali ya mambo katika Bahari Nyekundu, na kulifanya eneo hilo la majini kuwa la harakati za kijeshi.

Kiongozi huyo wa Ansarullah amesisitiza kuwa, mashambulio hayo ambayo ni sehemu ya operesheni za kuonyesha uungaji mkono wa Wayemen kwa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza yataendelea hadi pale utawala wa Kizayuni utakapositisha jinai zake na mauaji ya kimbari huko Gaza.

Image Caption

 

Huku hayo yakiripotiwa, vikosi vya ulinzi vya Yemen jana Alkhamisi vilifanya shambulio jipya la makombora dhidi ya meli ya kibiashara ya Uingereza katika maji ya Bahari Nyekundu; saa chache baada ya US na UK kufanya mashambulizi ya anga katika mkoa wa kaskazini wa Sa’ada na mji wa bandari wa al-Hudaydah, magharibi mwa Yemen.

Kabla ya hapo pia, Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree alisema vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vimefanya shambulio jingine la makombora dhidi ya meli ya kivita ya Marekani ya USS Gridley katika maji ya Bahari Nyekundu.

Vikosi vya ulinzi vya Yemen vimesema havitasimamisha mashambulizi yao hadi pale utawala haramu wa Israel utakapokomesha hujuma zake za kinyama dhidi ya Gaza, ambazo tangu Oktoba 7 hadi sasa zimeshateketeza roho za Wapalestina zaidi ya 27,000.

Tags