Feb 22, 2024 10:12 UTC

Vyanzo vya habari vya Kiebrania vimeonya juu ya hali ngumu itakayoikabili Israeli ikiwa itaanzisha vita dhidi ya Lebanon na uwezekano wa kuangamia maelfu ya Waisraeli, kufuatia vitisho vya mara kwa mara vya maafisa wa Israeli dhidi ya Lebanon na Hizbullah.

Eneo la mpaka wa Lebanon na kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, hivi karibuni limekuwa likishuhudia hali ya machafuko sambamba na kuendelea vitisho vya maafisa wa Israel vya kufanya mashambulizi makali dhidi ya Lebanon. Mivutano hiyo ilishadidi baada ya utawala wa Kizayuni kushambulia maeneo ya raia ndani ya Lebanon, na katika upande mwingine Hizbullah nayo ilijibu mapigo kwa kushambulia maeneo na ngome za jeshi la utawala huo ghasibu.

Kuhusiana na hilo, vyombo vya habari vya Kiebrania vimefichua ripoti rasmi kuhusiana na kadhia hiyo na kusema vitisho vya Tel Aviv vya kuishambulia Lebanon, vitaufanya utawala wa Kizayuni ukabiliwe na "mazingira magumu" iwapo utaanzisha vita na Lebanon; suala ambalo litasababisha vifo vya maelfu ya wagonjwa kutokana na kukatwa umeme wa maeneo mengi ya utawala huo.

Kuhusiana na jambo hilo, televisheni ya lugha ya Kiebrania Kan 11 imechapisha ripoti ya mwandishi wake wa kisiasa, Michael Shemes," ambayo imefichua mkanda wa sauti wa waziri wa afya wa Israeli akitahadharisha juu uwezekano wa Israeli kukabiliwa na hali mbaya na ya kutisha ambayo haijawahi kuhushuhudiwa katika historia yake iwapo itaingia vitani na Hizbullah.

Waziri huyu wa Kizayuni amezungumzia suala la kukatwa  umeme kwa muda mrefu katika maeneo yote ya kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, jambo ambalo linatia wasiwasi kuhusu uangalizi wa makumi ya maelfu ya wagonjwa wenye matatizo ya kupumua.

Kwa mujibu wa ripoti ya mtandao huo wa Kizayuni, Israel inajiandaa kwa ajili ya kukatika umeme wa zaidi ya asilimia 60 ya maeneo yake, hatua ambayo itaendelea kwa takriban masaa 48, na henda ikaendelea kwa wiki tatu katika baadhi ya maeneo.

Tovuti ya Israel ya Kan 11 imeendelea kusema kuwa, Moshe Bar Siman, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Israel, amesema kuhusiana na jambo hilo kuwa: Hali hiyo ngumu itafikia kiwango cha idadi kubwa ya Waisraeli kupoteza maisha.

Mtandao huo wa Kizayuni umeendelea kufichua kuwa, Wizara ya Afya ya Israel inaandaa mikakati ya ununuzi mkubwa wa jenereta za kuzalisha umeme na kuongeza: Kadiri wasiwasi na hofu inavyozidi kuongezeka katika eneo la kaskazini, ndivyo hatari ya Waisraeli inavyoongezeka, na wanatumai kutoshuhudia hali kama hiyo.

Vyombo vya habari vya Kiebrania vilevile vimeripoti kuwa tangu kuanza Operesheni ya Kkimbunga cha Al-Aqsa na kurushwa maroketi kutoka kusini mwa Lebanon, maafisa na wanajeshi kadhaa wa Israel wameangamizwa na makumi ya kambi za jeshi zimepigwa kwa makombora ya Hizbullah; kwa sababu hiyo, baraza la mawaziri lenye misimamo mikali la Benyamin Netanyahu limelazimika kuwahamisha maelfu ya walowezi kutoka maeneo ya kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na baadhi ya walowezi wameamua wao wenyewe kukimbilia maeneo mengine.

Maeneo ya walowezi wa Kizayuni

Hivi majuzi vyombo vya habari vya Israel vilifichua kuwa walowezi wa Kiziayuni hawako tayari kurejea makwao na kusema kuwa Baraza la Mawaziri la Netanyahu limewatelekeza.

Siku moja baada ya uvamizi wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba, Hizbullah ya Lebanon ilikuwa mhimili wa kwanza katika kambi ya Muqawama kujiunga rasmi na operesheni ya Wapalestina ya Kimbunga cha Al-Aqsa kwa kufanya mashambulizi kaskazini mwa Israel, na tangu wakakti huo mipaka ya Lebanon na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina imekuwa ikishuhudia mapigano ya kila siku na matukio ya kurushiana risasi kati ya vikosi vya Muqawama vya Lebanon na jeshi la Israel.

Tags