Mar 06, 2024 11:31 UTC
  • Ukosoaji wa UN wa mashambulizi ya makusudi ya Israel dhidi ya misafara ya misaada huko Gaza

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Chakula ametangaza kwamba, jeshi la Israel linashambulia kwa makusudi misafara ya misaada ya kibinadamu huko Gaza licha ya kujua njia za misafara hiyo.

Michael Fakhri amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel hautaki msaada wowote uwafikie watu wasiojiweza wa Gaza, na kwa kufanya hivyo, unasababisha baa la njaa kwa makusudi dhidi ya Wapalestina. Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Chakula ametoa wito wa kuwekewa vikwazo Israel kwa kupuuza maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) na kufanya uhalifu wa kivita huko Gaza.

Image Caption

Ukosoaji na onyo la wazi la afisa huyo wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhalifu unaofanywa na Israel huko Gaza hususan mashambulizi ya makusudi dhidi ya misafara ya misaada ya kibinadamu, kwa mara nyingine tena vinatukumbusha hali mbaya sana ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza huku tukikaribia kuingia mwezi wa sita wa vita vya Gaza. Israel, ikiwa na baraka kamili za Marekani kama muungaji mkono mkuu na muhimu zaidi wa utawala huo, imekuwa ikifanya mauaji ya halaiki dhidi ya wakazi wa Gaza katika miezi kadhaa iliyopita. Mbali na kulizingira kikamilifu eneo hilo la Palestina, Israel pia imewanyima wakazi wa eneo hilo haki za msingi kabisa za binadamu. Sehemu moja ya uhalifuu huo wa Israel ni kuwatesa watu wa Gaza kwa njaa. Kabla ya vita vya Gaza, kwa uchache robo ya wakazi wa eneo hilo walikuwa wakisumbuliwa na njaa; sasa hali hiyo imekuwa mbaya zaidi na watoto wengi wamekufa kutokana na njaa.

Kuhusiana na suala hili, Oxfam, ambalo ni shirika la kimataifa la misaada ya kupambana na umaskini, linasema kuwa mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada ya kibinadamu ni tabia na mtindo endelevu wa jeshi la Israel, ambao unazidisha mzozo wa usalama wa chakula huko Gaza. Msemaji wa Oxfam anasema: "Hali ni mbaya sana huko Gaza na kuna udharura wa kusitishwa mapigano mara moja ili kudhibiti tishio la njaa, kwani wakati unayoyoma."

Gaza

Licha ya hali hiyo mbaya, utawala wa Kizayuni unazidisha mashinikizo dhidi ya watu wa Gaza, ikiwa ni pamoja na kuzidisha mashambulizi na kuua watu wa eneo hilo, huku Marekani ikiendelea kutoa misaada ya kijeshi, kiuchumi na kisiasa kwa utawala huo. Rais wa Marekani, Joe Biden, ameendeleza sera za kinafiki na kindumakuwili za Washington kuhusu vita hivyo na kusema Israel inahitaji muda zaidi katika vita vya Gaza. John Kirby, mmoja wa maafisa wakuu wa Ikulu ya White House, pia ametangaza katika mkutano wake na waandishi wa habari kwamba: "Tutaendelea kufanya kazi na Israel ili kuhakikisha kuwa inaweza kujilinda na kufikia makubaliano katika suala mateka."

Wakati huo huo, uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa asilimia 52 ya Wamarekani wanataka serikali yao ikome kutuma silaha kwa utawala wa Israel. Uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na CEPR unaonyesha kuwa, Wamarekani wengi wanamtaka Biden aache mara moja kutuma silaha kwa Israel.

Ukosoaji wa wanasiasa wa sera za Joe Biden kuhusiana mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Gaza pia unaongeza sana baina ya wanasiasa wa Marekani kwenyewe. Kwa mfano tu, Seneta wa Kidemokrati, Elizabeth Warren, amekosoa sera ya Biden kuhusiana na mienendo ya Tel Aviv, akisema: "kama washirika wa Biden katika Congress, tunataka kumjulisha kwamba tabia na mienendo ya Netanyahu haina maslahi kwa Washington." Warren ametoa wito wa kufanyika mabadiliko katika sera ya Biden kuhusiana na Netanyahu.

Elizabeth Warren

Seneta mwingine wa chama cha Democratic, Chris Coons, pia ametangaza kwamba umewadia wakati wa kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Netanyahu kuhusiana na vita vya Gaza.

Hapana shaka yoyote kwamba, maadamu utawala wa Kizayuni wa Israel una uhakika wa kuendelea kupokea silaha na misaada ya kisiasa na kijeshi ya Marekani, si tu kwamba hautabadilisha mwelekeo wake katika vita vya Gaza, bali pia utazidisha jinai na uhalifu wake, ikiwa ni pamoja na kutumia njaa kama silaha ya vita vya Gaza, mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, pamoja na mashambulizi ya makusudi dhidi ya misafara ya misaada kwa lengo la kuzuia misaada ya kibinadamu kuwafikia watu wa Gaza.

Vitendo hivi ni mifano ya wazi ya uhalifu wa kivita, na wahusika wote wanapaswa kufunguliwa mashitaka na mamlaka husika za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.

Tags