Mar 07, 2024 02:29 UTC
  • Matokeo ya miezi 5 ya vita dhidi ya Gaza

Miezi 5 ya vita dhidi ya Ukanda wa Gaza ambavyo vilikuwa havijawahi kushuhudiwa tena imekuwa na matokeo mbalimbali katika ngazi ya ndani, kikanda na kimataifa.

Mwezi wa tano wa vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza ulimalizika Jumatatu tarehe 4 Machi, ambapo vita hivyo sasa vimeingia mwezi wa sita tokea kuanza kwake. Hadi sasa vita hivyo vimekuwa na athari katika nyanja tatu za ndani ,kieneo na kimataifa.

Ndani ya Gaza kwenyewe, vita hivyo vimesababisha mauaji ya halaiki. Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa katika kipindi hicho, Wapalestina 30,534 wameuawa shahidi na wengine 71,920  kujeruhiwa. Miundombinu ya Gaza pia imeharibiwa kabisa. Njaa ndiyo inatawala eneo la Gaza na kwa mujibu wa ripoti zinazotolewa, watoto wa Gaza sasa wanalazimika kula chakula cha wanyama. Licha ya machungu hayo yote, lakini muqawama wa wananchi wa Ghaza dhidi ya jinai za utawala haramu wa Kizayuni bado haujapungua na unaendelea kama kawaida. Mohammad al-Hindi, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesema kuhusiana na suala hilo kuwa, utawala wa Kizayuni umeshindwa kuangamiza muqawama wala kuwakomboa mateka wake wanaoshikiliwa na wapiganaji wa Kiislamu huko Ghaza. Katika kipindi cha miezi mitano iliyopita utawala wa kigaidi wa Israel umeshindwa kufikia malengo uliyotangaza mwanzoni mwa vita, na hivi sasa umeanzisha operesheni ya mauaji ya kimabari katika ukanda huo.

Kikao cha Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni

Ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwenyewe (Israel), migawanyiko, hitilafu na mivutano kati ya Baraza la Mawaziri la Netanyahu na Baraza la Mawaziri la Vita la utawala wa Kizayuni imedhihirika hadharani na si jambo la siri tena. Maandamano yameongezeka katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ambapo waandamanaji wanataka kuvunjwa baraza la mawaziri. Aidha matatizo ya kiuchumi ya utawala huo hususan ukosefu wa ajira nayo yameongezeka. Uhamiaji  kutoka ardhi zinazokaliwa kwa mabavu pia umeongezeka. Tokea kujiri kimbunga cha Al Aqsa operesheni za kijasusi za Israel zimekuwa zikifeli mara kwa mara kufuatia kushindwa utawala wa Kizayuni kuwaachilia huru mateka wake.

Katika ngazi ya kieneo, vita vya Ghaza vimepelekea kuwekwa kando suala la Palestina na nchi za Kiarabu. Licha ya kuendelea mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza, nchi za Kiarabu hazijatoa mashinikizo yoyote mahimu kwa utawala huo ili usimamishe jinai zake dhidi ya watu wasiokuwa na hatia wa Ghaza. Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu nayo haijachukua hatua yoyote isipokuwa kufanya vikao visivyokuwa na maana. Kuhusiana na suala hilo, Yemen ambayo ilipitia kipindi cha miaka 8 ya vita vya kidhalimu vya Saudia dhidi yake, ndiyo imechukua hatua athirifu ya kushambulia na kuzizuia meli zinazoelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hatua hiyo imeuzidishia matatizo ya kiuchumi utawala wa Kizayuni na wakati huo huo kutilia shaka madai ya haki za binadamu yanayotolewa na Marekani kwa sababu imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya Yemen ili kuunga mkono mauaji ya kimbari ya utawala huo wa Kizayuni. Hizbullah ya Lebanon nayo pia kwa kufanya mashambulizi upande wa kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu imejaribu kuelekeza baadhi ya operesheni za utawala huo katika maeneo hayo, na hivyo kupunguza mashinikizo ya utawala huo dhidi ya watu wa Ghaza.

Uharibifu mkubwa wa vita vya Ghaza

Kimataifa, utawala wa Kizayuni umepata hasara na madhara makubwa kuhusiana na vita vya Ghaza. Marekani na madola matatu ya Ulaya, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zimepata hasara kubwa zaidi kwa sababu ya siasa zao za kuunga mkono rasmi mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza. Marekani imepiga kura ya turufu dhidi ya maazimio yote yaliyopendekezwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kusimamisha vita huko Ghaza na kudai rasmi kwamba hatua za mauaji na jinai za utawala wa Kizayuni ni za kujilinda. Umoja wa Mataifa pia umepata pigo kubwa katika vita hivyo kwa sababu umeshindwa kuvisimamisha wakati jukumu muhimu zaidi la Baraza la Usalama la umoja huo ni kulinda, kudumisha na kuimarisha amani na usalama duniani. Pamoja na hayo lakini  kura ya turufu ya Marekani imelipelekea baraza hilo kupooza na kutochukua hatua yoyote ya maana katika uwanja huo.

Hivi sasa mgogoro wa Ghaza umeingia katika mwezi wake wa sita kukiwa hakuna matumaini yoyote ya kumalizika hivi karibuni.

Tags