Mar 28, 2024 09:32 UTC
  • Subira ya kihistoria ya watu wa Ghaza, sababu kuu ya kufedheheka Israel duniani

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwenye mazungumzo yake na Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kwamba, subira ya kihistoria na kusimama imara wananchi wa Ghaza mbele ya jinai za utawala wa Kizayuni kumeifanya kadhia ya Palestina kuwa suala kuu nambari moja duniani.

Kwa kkaribu miezi sita sasa utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya mauaji ya umati dhidi ya wananchi wa Ghaza na licha ya kuuawa shahidi na kujeruhiwa karibu Wapalestina laki mja na 8,000 na kutojulikana waliko karibu watu 8,000 wengine na pamoja na kuweko wakimbizi karibu Wapalestina milioni 2, lakiini bado utawala wa Kizayuni umeshindwa kufikia malengo yake ya kijeshi uliyotangaza kuwa ndiyo sababu ya kuanzisha vita vikubwa dhidi ya wananchi wa Ghaza. Malengo yaliyotangazwa na utawala wa Kizayuni ni kuwakomboa mateka wa Kizayuni na kuiangamiza HAMAS bali hata kuikalia tena kwa mabavu Ghaza lakini umeshindwa kufikia malengo hayo.

Israel hadi hivi sasa imeshindwa kuwakomboa mateka Wazayuni huku familia za mateka hao zikizidi kuishinikiza serikali ya viongozi makatili wa Kizayuni inayoongozwa na Netanyahu. Vita hivyo vimeshindwa kuipigisha magoti HAMAS na hivi sasa Tel Aviv imelazimika kukubali kufanya mazungumzo na HAMAS kuiomba iwaachilie huru mateka hao. Ndani ya mazungumzo, HAMAS imekataa masharti ya kubebeshwa na ya kuburuzwa ya Wazayuni na imetoa masharti mazito kwa utawala wa Kizayuni kama unataka kweli mateka hao waachiliwe huru.

Utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake hasa Marekani wamefedheheka duniani kutokana na jinai zao za kutisha dhidi ya Wapalestina

 

Kuingamiza Harakati ya Mapambnao ya Kiislamu ya Palestina ndilo lengo jingine la Israel la kuivamia kijeshi Ghaza hivi sasa lakini si tu lengo hilo halijafikiwa, lakini utawala wa Kizayuni umelazimika kukimbilia kwa wapatanishi wa kieneo na nje ya eneo hili ili iweze kufanya mazungumzo na harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu, suala ambalo lina maana kuwa Israel inakiri kuwa HAMAS bado ina nguvu na haiwezi kuiangamiza.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na kituo cha utafiti wa kisiasa na maoni ya Wapalesina ambacho ni kituo takriban cha watu wasiopenda dini na kiko chini ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina unaonesha kuwa, asilimia 70 ya Wapalestina wanaiunga mkono HAMAS kutokana na hatua zake za kupigania ukombozi wa Palestina na operesheni yake ya Kimbunga cha al Aqsa ya tarehe 7 Oktoba 2023. Asilimia 71 ya Wapalestina wamesema kuwa operesheni ya HAMAS ya Kimbunga cha al Aqsa ilikuwa sahihi na ilipaswa ifanyike ili kuiokoa kadhia ya Palestina.

Lengo jingine la utawala wa Kizayuni ni la kutaka kuukalia tena kwa mabavu Ukanda wa Ghaza. Lengo hilo nalo halijafikiwa kwani Ghaza ni sehemu muhimu sana ya utambulisho wa Palestina, na hata itokezee eneo lote hilo lishambuliwe na isibakie hata nyumba moja, Wapalestina lazima watarejea Ghaza. Mtazamo huo usioyumba kuhusu Ghaza umewafanya wakazi wa ukanda huo waoneshe subra ya kihistoria ambayo imepongezwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye amesema kuwa, subira hiyo ya kihistoria ya watu wa Ghaza ndiyo sababu kuu ya kufedheheka utawala wa Kizayuni duniani. 

Nukta nyingine muhimu hapa ni kwamba, subira ya wananchi wa Ghaza mbele ya jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni imepelekea walimwengu wazidi kutambua uhalisia wa kikaktili na kkijinai wa utawala wa Kizayuni na hivi sasa Israel inachukiwa mno duniani tena kwa kukiri viongozi wenyewe wa madola ya Magharibi ambao ni waungaji mkono wakuu wa utawala wa Kizayuni. Mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi watu wa Ghaza yameamsha hisia za kila mtu mwenye fikra za kibinadamu duniani na kuwa jinamizi jingine kwa Israel ambayo miaka yote hii ilikuwa inajifanya ni taifa lililodhulumiwa na linalopenda amani na usalama kwa watu wote.