Apr 01, 2024 11:22 UTC
  • Hamas: Kuanzisha maeneo ya kunyonga watu huko Gaza ni uhalifu wa kikatili wa kivita

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema kwamba, kilichofichuliwa na vyombo vya habari vya Israel kuhusu hatua ya jeshi la utawala huo ya kuanzishwa "maeneo ya kunyonga watu" katika Ukanda wa Gaza, ambapo mtu yeyote anayetembea katika maeneo hayo anauawa, ni jinai ya kikatili ya kivita.

Taarifa iliyotolewa na Hamas imeongeza kwamba, vitendo hivi vya Israel ni kielelezo cha "ukiukaji wa kanuni na sheria zote za vita kwa kuwalenga raia wasio na silaha katika matukio ambayo baadhi yamefichuliwa katika video zilizotangazwa hapo awali na televisheni ya Al Jazeera."

Jumatano iliyopita, televisheni ya Al Jazeera ya Qatar ilionyesha mkanda wa video ya wanaume wawili wa Kipalestina wasio na silaha, mmoja akipeperusha hewani kitambaa cheupe kama ishara ya kujisalimisha, kabla ya askari katili wa jeshi la Israel kuwapiga risasi na kisha kuzifukia maiti zao kwenye kifusi kwa kutumia tingatinga, karibu na mji wa Gaza.

Raia wa Palestina akishikiliwa na wanajeshi wa Israel

Majuzi pia vyombo vingine vya habari vilifichua video nyingine ambazo zinaonyesha mauaji ya kimakusudi ya Israel dhidi ya raia wasio na silaha wa Palestina huko Gaza.

Hamas imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa na taasisi za mahakama za kimataifa - zikiongozwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu - kuanza uchunguzi wa haraka kuhusu uhalifu huo wa kutisha unaoonekana kwa sauti na video mbele ya ulimwengu mzima.

Pia imetoa wito wa kufunguliwa mashitaka viongozi wa utawala vamizi na wa Kinazi wa Israel, kufanya kazi ya kukomesha mauaji ya utawala huo na vita vya maangamizi vinavyoendelea dhidi ya raia wasio na ulinzi, na kulinda maadili ya ubinadamu yanayokanyagwa na utawala huo kwa baraka na mwanga wa kijani kutoka kwa utawala wa Rais wa Marekani, Joe Biden.

Jana Jumapili, maafisa na wanajeshi wa Israel walikiri kwamba wengi kati ya waliouawa, ambao jeshi liliwataja kuwa magaidi kwenye vita vya sasa huko Ukanda wa Gaza, kwa hakika walikuwa raia wasio na silaha.

Gazeti la Israel la Haaretz limekusanya ushuhuda kutoka kwa maafisa hao na wanajeshi waliopigana vita ambavyo vinaendelea tangu Oktoba 7, 2023.

Tags