Apr 13, 2024 11:51 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu ongezeko la magonjwa ya kuambukiza katika Ukanda wa Gaza

Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesema: magonjwa ya kuambukiza yanaenea katika Ukanda wa Gaza kutokana na ukosefu wa maji salama na kuongezeka kwa joto.

Jamie McGoldrick, mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba: "Joto linaongezeka katika eneo la Ukanda wa Gaza, na watu wanapata maji kidogo kuliko wanavyohitaji, matokeo yake, kunajitokeza magonjwa ya kuambukiza kupitia maji kutokana na ukosefu wa maji salama na uharibifu wa mfumo wa maji taka.

Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, aliyekuwa akizungumza baada ya ziara yake ya hivi majuzi katika Ukanda wa Gaza, ameongeza kuwa: "Katika miezi ijayo, kutakuwepo ulazima wa kutafuta njia ya kudhamini maji salama katika maeneo yenye msongamano wa watu ambako watu wamekusanyika kwa sasa."

Gaza

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, maji machafu na mifumo duni ya afya vinahusishwa na magonjwa kama vile kipindupindu, kuhara, kuhara damu na homa ya ini.

Kabla ya hapo msemaji wa Shirika la Afya Duniani alikuwa amesisitiza kuwa, iwapo mfumo wa afya wa Gaza hautatengenezwa haraka, basi hatari ya vifo vinavyotokana na maradhi kwa wakazi wa eneo hilo itakuwa kubwa zaidi kuliko mashambulizi ya mabomu ya ndege za kivita za wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tags