Apr 14, 2024 13:11 UTC
  • Uamuzi wa Pakistan dhidi ya harakati ya Zainabiyyun; malengo na matokeo yake

Serikali ya Pakistan imechukua uamuzi wa kushtukiza na uliowashangaza na kuwapiga butwaa watu wengi, nao ni wa kuiweka harakati ya Zainabiyyun kwenye orodha yake ya tasisi za kigaidi licha ya kwamba harakati hiyo muda wote imekuwa ikipigania amani na usalama kwa Pakistan.

Tunapoangalia historia ya hadi hivi sasa na harakati ya Zainabiyyun tutaona kuwa, kamwe haijawahi kuchukua hatua yoyote ya kuhatarisha usalama na amani kwenye eneo hili ikiwemo Pakistan, bali katika kipindi cha muongo mmoja cha kuasisiwa kwake, muda wote imekuwa ikipigania usalama wa eneo hili zima. Zainabiyyun inaendesha harakati zake nchini Syria na lengo lake ni kupambana na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) na imepata mafanikio makubwa sana katika suala hilo.

Baada ya magenge ya kigaidi kuivamia ardhi ya Syria kutoka kila kona ya dunia, vijana wa Pakistan walijikusanya pamoja na kuanzisha taasisi ya Zainabiyyun kwa ajili ya kwenda kulinda maeneo matakatifu huko Syria. Muongo mmoja umepita tangu taasisi hiyo ianzishwe na muda wote imekuwa ikitangaza hadharani kwamba lengo lake ni kukabiliana na magenge ya kigaidi tena nchini Syria. 

Harakati ya Zainabiyyun

 

Taasisi hiyo iliasisiwa ikiwa na wanachama 24 tu. Baada ya hapo vijana mbalimbali walijitokeza kujiunga nayo na hivi sasa inajulikana kwa jina maarufu la Jeshi la Zainabiyyun. Harakati hiyo imeshiriki kwenye operesheni mbalimbali kama za ukombozi wa Halab, Nubl na Al Zahraa, Tadmur, Hama na maeneo ya kwenye viunga vya mjini mkuu wa Syria, Damascus. Hata baada ya kukombolewa maeneo hayo, kikosi cha Zainabiyyun kimekuwa na mchango mkubwa katika juhudi za kurejesha hali ya mambo kuwa ya kawaida kwenye maeneo hayo. Wanamapambano wa Zainabiyyun walikuwa mstari wa mbele na ngao imara kwenye operesheni ya Boukamal iliyoongozwa na Luteni Jenerali Qassem Soleimani, operesheni ambayo ilipelekea kuangamizwa na kufutwa kabisa genge la Daesh katika eneo hilo la nchini Syria.

Ali Zahedi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Vikosi vya wapiganaji kama cha Zainabiyyun viliingia kupambana na magaidi wa Daesh huko Syria baada ya genge hilo kukua na kugeuka kirusi na donda la kensa ambalo lilikuwa linahatarisha usalama wa dunia nzima. Lau kama vikosi kama hivyo vya kujitolea visingelikuwepo, hivi sasa magaidi wa ISIS wangekuwa wana nguvu kwenye eneo hili mpaka Pakistan kwenyewe. Hasa kwa kutilia maanani pia kwamba hata hivi sasa bado mabaki ya magaidi wa Daesh yanafanya vitendo vya kigaidi ndani ya Pakistan, na serikali ya nchi hiyo inalazimika kutumia nguvu za ziada kukabiliana nayo.

Walichokitarajia wananchi wa Pakistan ni kuona serikali yao na jeshi la nchi hiyo linatumia vizuri uzoefu wa wapiganaji wa Zainabiyyun katika kukabiliana na magaidi wa Daesh ndani ya Pakistan na sio kufanya kinyume kabisa na ilivyotarajiwa na kila mtu. Muhimu zaidi kuliko yote ni kwamba harakati ya Zainabiyyun haijawahi kufanya kitendo chochote cha kuhatarisha usalama wa eneo hili na si Pakistan pekee; bali muda wote inapigania kuweko usalama, utulivu na amani katika eneo hili zima.

Harakati ya Zainabiyyun ni ya kujitolea ya wananchi wa kawaida. Inashangaza sana kuona serikali ya Pakistan imeiweka kwenye orodha yake ya makundi ya kigaidi.

 

Ndio maana katika majibu yake, harakati ya Zainabiyyun ikawakhutubu wanasiasa na viongozi wa Marekani ikiwaambia: Bila ya shaka yoyote habari ya mapambano ya kishujaa ya jeshi la Zainabiyyun katika kulinda Haram za Ahlul Bait AS nchini Syria mumezisikia. Hivyo mnapaswa kuelewa kwamba neno woga halimo kabisa kwenye kamusi ya mapambano ya Kiislamu. Maamuzi na mtazamo wa kihabithi wa Marekani na vitimbakwiri vyake haviwezi kufanya lolote ghairi ya kuzidisha umoja na mshikamano katika safu za wanamapambano wa Kiislamuu. 

Amma hatua ya serikali ya Pakistan ya kuiweka harakati ya Zainabiyyun kwenye orodha ya makundi ya kigaidi inaweza kutathminiwa katika hali kadhaa. Miongoni mwake ni kwamba hatua hiyo imechukuliwa mara baada ya waziri mkuu wa Pakistan, Shahbaz Sharif kutembelea Saudia Arabia. Pili inavyoonekana ni kuwa, serikali mpya ya Pakistan inataka kupunguza mivutano na Marekani na kuomba msaada wa kiuchumi na kijeshi kutoka kwa Washington. Lakini tatu ni kwamba, hatua hiyo kamwe haiwezi kukubaliwa na wananchi wa Pakistan hasa kwa kuzingatia jinsi utawala wa Kizayuni unavyofanya mauaji ya kimbari huko Ghaza na namna utawala huo unavyoziogopa sana taasisi za Kiislamu ikiwemo hiyo ya Zainabiyyun.

Tags