Apr 16, 2024 10:48 UTC
  • Wazayuni wanakwepa kurejea maeneo wanayoishi kwa kuhofia mashambulio ya Hizbullah

Televisheni ya utawala wa Kizayuni wa Israel imefichua kuwa, sehemu kubwa ya Wazayuni wanaoishi kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni, wanakwepa kurejea maeneo hayo wakihofia mashambulio ya Hizbullah ya Lebanon.

Kanali ya 12 ya televisheni ya Israel imesema kuwa, baada ya kupita zaidi ya miezi 6 ya vita dhidi ya Ukanda wa Ghaza, asilimia 40 ya wakazi wa maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazopakana na Lebanon wanakwepa kurejea kwenye sehemu hizo kwa kuogopa mashambulizi ya Hizbullah. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 27 ya watu waliokuwa na kazi huru hivi sasa wanapanga kuhama kabisa maeneo hayo na kuhamia sehemu nyingine kuendelea na biashara zao.

Televisheni hiyo ya Kizayuni aidha imefichua kuwa, asilimia 73 ya kazi za watu binafsi zimepotea katika ardhi za kaskazini mwa Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni tangu mwezi Oktoba mwaka jana ilipoanza operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa na hali ya uchumi ya maeneo hayo imeporomoka kabisa.

Hizbullah ya Lebanon ilianzisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, baada ya utawala wa Kizayuni kuanzisha mauaji ya umati dhidi ya wananchi wa Ghaza. Kila siku Hizbullah inafanya mashambulizi kwenye maeneo hayo na kuwalazimisha Wazayuni wengi kukimbilia maeneo mengine au kupanda ndege na kukimbilia nje kabisa ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni kutokana na kushindwa kuvumilia mashambulizi ya wanamapambano wa Kiislamu. 

Tags