Apr 17, 2024 10:49 UTC
  • Wapalestina 16 wa Ukanda wa Ghaza wameuawa shahidi kwenye jela za utawala wa Kizayuni

Kamati inayoshughulikia masuala ya Wapalestina wanaoshikiliwa na walioachiwa huru kutoka kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel imetangaza kuwa, mateka 16 wakazi wa Ukanda wa Ghaza wameuawa shahidi wakiwa wanashikiliwa kwenye magereza ya utawala huo.

Kamati hiyo imetangaza leo kuwa, tangu vilipoanza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza tarehe 7 Oktoba 2023 hadi sasa, wafungwa 16 wakazi wa ukanda huo wameuawa shahidi katika jela za utawala huo kutokana na mateso.
 
Kamati inayoshughulikia masuala ya Wapalestina wanaoshikiliwa na walioachiwa huru kutoka kwenye magereza ya Wazayuni imeongeza kuwa, licha ya wafungwa wa Kipalestina kuendelea kuteswa katika jela za utawala wa Kizayuni, dunia imeendelea kukaa kimya na kuwa kitu kimoja na utawala huo ghasibu.
 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wananchi wa Palestina wanakabiliwa na mashambulizi na jinai za walowezi maghasibu wa Kizayuni waliojizatiti kwa silaha, wanaotekeleza moja kwa moja amri za utawala wa Kizayuni.

Tangu vilipoanza vita vya Ghaza, Wapalestina wasiopungua elfu tatu wakazi wa eneo hilo wamekamatwa na jeshi la Kizayuni na kutiwa magerezani.

 
Kuanzia Oktoba 7, 2023, na kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi, utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya mauaji makubwa katika Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya wananchi madhulumu na wasio na ulinzi wa Palestina, na kimya kinachoonyeshwa na jamii ya kimataifa na asasi za kutetea haki za binadamu kwa jinai za Israel kimekuwa sababu ya utawala huo haramu kuendeleza mauaji ya wanawake na watoto wa Kipalestina.
 
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, tangu zilipoanza jinai hizo za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza tarehe 7 Oktoba hadi sasa, zaidi ya Wapalestina 33,843 wameuawa shahidi na zaidi ya wengine 76,575 wamejeruhiwa, ambapo akthari ya waathirika wa mashambulizi hayo ni wanawake na watoto.../

 

Tags