Harakati za muqawama wa Palestina: Hatutashiriki katika mazungumzo yoyote na utawala wa Kizayuni
Harakati za Mapambano za Palestina za Hamas na Jihadul Islami zimetangaza kuwa hazitashiriki tena kwenye mazungumzo yoyote baada ya utawala wa Kizayuni kushambulia kambi ya wakimbizi wa Kiaplestina katika mji wa Rafah.
Utawala wa Kizyauni juzi usiku ulishambulia zaidi ya mahema na vituo kumi vilivyokuwa makazi ya wakimbizi wa Kipalestina katika mji wa Rafah na kuwaua shahidi Wapalestina zaidi ya 190 wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi makumi ya wengine.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Harakati za Mapambano za Palestina za Hamas na Jihadul Islami jana Jumatatu zilitoa taarifa tofauti zikilaani mauaji hayo yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni kaskazini magharibi mwa mji wa Rafah. Hamas na Jihadul Islami zimezitaja jinai za Israel kuwa ni upuuzaji wa wazi wa uamuzi wa karibuni wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) juu ya ulazima wa kusitisha mashambulizi katika mji huo. Harakati za muqawama za Palestina pia zimemtaja Rais Joe Biden wa Marekani na serikali ya nchi hiyo kuwa wahusika wa jinai hizo.
Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imetoa taarifa ikilaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya kambi za wakimbizi wa Kipalestika katika mji wa Rafah na kusisitiza kuwa kuna ulazima wa utawala wa Kizayuni kuheshimu uamuzi wa mahakama ya ICJ ulioutaka usimamishe mashambulizi katika mji huo.
Wizara ya Afya ya Palestina wakati huo huo imetangaza kuwa utawala wa Kizayuni juzi ulitekeleza jinai mpya saba katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza na kuuwa shahidi watu 66 na kuwajeruhi wengine 383.