Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu-2
Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur´ani, kuwa mwongozo kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi atayekuwa katika mji (wake) katika mwezi huu aufunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amewangoza ili mpate kushukuru. (Baqarah:185)
Tumo katika mwezi ambao ni msimu wa machipuo wa ibada, mwezi ambao milango ya rehema ya Mungu inafunguliwa kwa waja wake, na mwezi ambao ni fursa ya kipekee ya kurudi kwenye utu wetu halisi. Ramadhani ni mwezi ambao roho za binadamu zinasafishwa na kuuwa mpya, na kumulikiwa na nuru ya Mwenyezi Mungu, na ndani yake wanadamu wanapewa fursa ya kurekebisha yaliyopita na kujikurubisha kwa Mungu.
Mwezi mtukufu wa Ramadhani umechaguliwa kwa ajili ya mfungo kwa sababu ya fadhila na sifa zake maalumu ikilinganishwa na miezi mingine ya mwaka. Ni mwezi ambao ndani yake Qur'ani Tukufu iliteremshwa. Vitabu vingine vitakatifu pia viliteremshwa katika siku za mwezi huu. Hata hivyo inatupasa kuelewa kuwa, Qur'ani si kitabu cha kawaida.
Je, umewahi kufikiria, Qur'ani ina hakika gani adhimu? Qur'ani sio kitabu cha maneno na misemo tu, bali ni hakika iliyo hai ambayo katika ulimwengu wa Akhera hubadilika na kuwa sura kama za Manabii, Malaika na waja wanaostahiki wa Mungu; Huzungumza na kuwa mwombezi na shafii kwa Mola Muumba. Qur'ani ni mwombezi ambaye uombezi wake unakubaliwa, msemakweli na msadikishaji, na kwa hakika ni miale ya nuru ya Mwenyezi Mungu. Ni kitabu chenye elimu ya yaliyopita na yajayo, elimu ya mwanzo na mwisho, elimu ya kumjua Mungu, Malaika na vitabu vya awali vya mbinguni, na hata uhakika wa ulimwengu na vilivyomo.

Ukweli huu wenye kina kirefu unaweza kuonekana katika maneno ya Ahlul-Bayt (as), watu adhimu ambao daima wamefuatana na kuilinda Qur’ani. Wanatukumbusha kwamba Qur’ani si kitabu tu, bali ni miale ya nuru ya Mwenyezi Mungu ambayo inamulikia wanadamu. Kitabu hiki cha Mwenyezi Mungu kina maarifa ya nyakati zilizopita na zijazo na ni taa inaonyesha njia ya saada na ufanisi wa milele. Katika baadhi ya daraja za ujudi na uwepo, hakika ya Qur'an imefungamana na hakika ya ujudi na uwepo Mtume Muhammad (saw) na warithi wake maasumu. Kama ambavyo Imam Ali (as) aliyosema: Mimi ni Qur’ani inayosema.
Kauli hii inaashiria kuwa Qur’ani ni hakika iliyohai na inayosema na kuzungumza na watu, na ina mfungamano usioweza kukatika na ujudi na uwepo wa Mtume (SAW) na Ahlubaiti zake watoharifu (as). Mwenyezi Mungu SW anasema katika Aya ya 79 ya Suratul Waqi’a kwamba:
لّا یَمَسُّهُ إِلاَّ الْمُطَهَّرُونَ
"Hapana akigusaye ila waliotakaswa." Baadhi ya wafasiri wa Qur’ani wanasema, maana yake ni kwamba, ili kuweza kuidiriki na kuielewa ipasavyo Qur’ani tunapaswa kuwa na nyoyo safi na zilizotakasika. Hivyo basi tunapoisoma Qur’ani tunapaswa kwanza kusafisha na kutakatisha nyoyo zetu, kuwa hadhir na makini wakati tunasoma Aya za kitabu hicho, na kutafakari kwa kina katika yanayosemwa na Allah SW.
(

Kusoma Qur’ani ni miongoni mwa matendo muhimu na yenye thamani kubwa ambayo yametengewa malipo na thamani kubwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mtume (saw) amesema kuhusiana na malipo ya kusoma Qur’ani katika mwezi huu kwamba: “Mwenye kusoma Aya moja ya Qur’ani katika mwezi huu atapata ujira wa aliyehitimisha Qur’ani nzima katika miezi mingine."
Hadithi nyingine imepokewa kwamba: "Muumini anayesoma Aya kumi za Quran kila usiku hataandikwa miongoni mwa "walioghafilika." Na ikiwa atasoma Aya hamsini kila usiku, jina lake litaandikwa miongoni mwa Dhakirina (wanaomkumbukwa Mwenyezi Mungu). Na kama atasoma Aya mia moja, jina lake litaandikwa miongoni mwa "Qaanitin" (waja safi na wanyenyekevu). Na ikiwa atasoma Aya mia moja kila usiku, jina lake litaandikwa miongoni mwa "waliofaulu". Akisoma Aya mia tano, jina lake litaandikwa miongoni mwa “Mujtahidin” (wale wanaofanya bidii na jitihada kubwa katika njia ya haki)......
Hadithi hizi zinatuonyesha kuwa mwezi wa Ramadhani ni fursa ya kuongeza ibada na kufaidika na malipo makubwa ya kusoma na kutadabari maana ya Qur’ani katika mwezi huu. Shime basi ndugu zangu! Katika mwezi huu uliobarikiwa, tujikurubishe zaidi kwenye radhi za Mwenyezi Mungu kwa kusoma Qur’ani na kutekeleza majukumu yetu ya faradhi, kwa kutumia vyema fursa za kipekee za siku hizi.
Katika dua ya siku ya pili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, tunasoma: "Ewe Mwenyezi Mungu, nikurubishe kwenye radhi zako ndani ya mwezi huu, na uniepushe na ghadhabu na aqama zako ndani yake, na nijaalie niweze kuzisoma Aya zako ndani yake kwa rehema zako, ewe mwingi wa kurehemu."
Dua hii iliyopokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (SAW) ni moja ya hazina zetu za kiroho katika siku hizi. Katika dua hii, tunamuomba Mola Mlezi atusogeze karibu na yale yanayompendeza, na atuepushe na kila kitu kinachotuweka mbali Naye.
Dua za mwezi wa Ramadhani, licha ya kuwa fupi, lakini zina maana kubwa na pana sana. Maombi haya yanatufundisha kwamba, katika mwezi huu, hatupaswi kufunga na kujizuia kula na kunywa tu, bali pia tupige hatua na harakati kwenye njia ya Allah na kumtafuta Yeye SW.

Njia bora ya kupata radhi za Mungu ni kutekeleza majukumu ya faradhi na kuacha na kujitenga na mambo yaliyoharamishwa. Hapa ni muhimu sana kuzingatia kwa undani kila moja ya matendo yetu. Imeelezwa katika Hadithi kwamba, wakati mwingine mtu hufanya kitendo kidogo, na Mwenyezi Mungu humsamehe dhambi zake zote kwa sababu ya kitendo hicho kiduchu. Kwa upande mwingine, mtu anaweza kufanya kitendo kiovu ambacho ni kidogo na kisicho na maana machoni pake mwenyewe, lakini Mungu anasema, "Naapa kwa utukufu wangu, kwamba sitasamehe kitendo hiki." Kwa sababu mtu huyo amepuuza na kuidogesha dhambi yake na hakufikiria kamwe kuirekebisha au kutubu dhambi hiyo.
Amirul-Mu’minina, Ali (AS), pia amesema kuhusu jambo hili kwamba: “Mwenyezi Mungu ameficha radhi yake katika utiifu. Basi usikitambue kitendo chochote cha twaa na utiifu kuwa ni kidogo, kwani pengine kina radhi na ridhaa ya Mwenyezi Mungu, na wewe hujui.”
Abu Abdullah Al Swadiq (as) amehadithia kwamba: Mtume (saw) alisimama katika ardhi tupu isiyo la chochote, na akawaambia maswahaba zake: Kusanyueni kuni. Walimwambia: Yaa Rasulallah! Tuko kwenye ardhi tupu isiyo na chochote na haina kuni. Mtume alisema: Kila mmoja wenu alete kiwango anachoweza kukusanya. Kila mmoja wao alipeleka kiwango cha kuni alichoweza kupata na kuziweka mbele ya Mtume (saw) katika rundo moja. Mtume aliwaambia: "Hivi ndivyo madhambi yanavyokusanyika. Kisha akasema: Jihadharini na madhambi madogo, kwani kila kitu kina mtafutaji, na mtafutaji wa madhambi haya anaandika 'waliyoyatanguliza na wanayoyaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha."
Amirul-Mu'minina Ali bin Abi Twalib pia amesema: "Dhambi mbaya zaidi ni ile inayodogeshwa na mtendaji wake", kwa maana ya mtu kuiona dhambi aliyotenda kuwa ni kitu kidogo. XXXXX