Kukombolewa Halab ni ushindi mkubwa na wa kistratejia
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i21430-kukombolewa_halab_ni_ushindi_mkubwa_na_wa_kistratejia
Kufuatia kukombolewa kikamilifu mji wa Halab au kwa jina jingine Aleppo kutoka mikononi mwa magaidi wa kitakfiri, wakazi wa mji huo siku ya Jumanne walimiminika mabarabarani na mitaani kusherehekea kwa vifijo na nderemo ushindi huo mkubwa na wa kistratijia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 15, 2016 00:37 UTC
  • Kukombolewa Halab ni ushindi mkubwa na wa kistratejia

Kufuatia kukombolewa kikamilifu mji wa Halab au kwa jina jingine Aleppo kutoka mikononi mwa magaidi wa kitakfiri, wakazi wa mji huo siku ya Jumanne walimiminika mabarabarani na mitaani kusherehekea kwa vifijo na nderemo ushindi huo mkubwa na wa kistratijia.

Baada ya kukombolewa mji huo wote, sasa ni sehemu chache tu katika mikoa ya Deir az-Zur ulio mashariki na ar-Raqqa ulioko kaskazini mwa Syria ndizo zingali zinadhibitiwa na magaidi ambapo inatazamiwa kuwa maeneo hayo pia yatakombolewa hivi karibuni kwa kutilia maanani motisha na moyo wa kupigana walionao hivi sasa askari jeshi wa nchi hiyo katika medani ya vita. Tokea mwaka 2012 mji wa Halab ulikuwa umegawanyika sehemu mbili za Magharibi na Mashariki ambapo upande wa Magharibi ulikuwa unadhibitiwa na akari wa serikali na ule wa mashariki ukidhibitiwa na magenge ya kigaidi yakiungwa mkono na nchi za Magharibi na Kiarabu. Tokea kuanza kwa mgogoro wa nchi hiyo  hatima ya Halab imekuwa na nafasi muhimu katika kuainisha mustakbali wa Syria. Kwa hakika mji wa Halab katika miaka ya hivi karibuni ulikuwa umebadilika na kuwa ngome kuu ya vita nchini Syria ambapo waungaji mkono wa makundi ya kigaidi wamekuwa wakitumia kila mbinu kuendelea kuudhibiti mji huo ili kuainisha mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo.

Wakazi wa Aleppo wakishangilia kukombolewa kwa mji huo na jeshi la taifa

Lakini sasa kwa kukombolewa mji huo mahesabu ya wafadhili hao wa ugaidi yamevurugika. Kukombolewa Halab, ambao ni mji wa pili kwa umuhimu na mkubwa zaidi kaskazini mwa Syria, kumetimia katika hali ambayo nchi zinazounga mkono ugaidi yaani serikali za Magharibi na baadhi ya serikali za Kiarabu za eneo zimetumia uwezo wao wote kutekeleza mipango na njama dhidi ya serikali halali ya Rais Bashar al-Asad wa nchi hiyo. Moja ya njama hizo ilikuwa ni kutaka kuasisi serikali ya magaidi na wapinzani wa serikali ya Damascus katika mji huo ili kuandaa uwanja wa kuigawa Syria sehemu mbili kwa msingi wa mpango wa Marekani wa eti kubuni Mashariki ya Kati Mpya katika eneo. Kwa msingi huo umuhimu wa ushindi wa kukombolewa Halab unaweza kulinganishwa na ule wa Hizbullah ya Lebanon mwaka 2006 katika vita vya siku 33 ambapo utawala haramu wa Israel ulianzisha uchokozi dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu. Katika vita hivyo pia utawala wa Kizayuni kwa niaba ya Marekani ulikuwa ukifuatilia mpango wa kuigawa Lebanon katika sehemu kadhaa kwa msingi wa Masharikiya Kati Mpya, mpango ambao ulishindwa  kutokana na mapambano ya wananchi shupavu wa Lebanon.

Magaidi wa Daesh kabla ya kufurushwa mjini Aleppo

 

Mtazamo wa kimaslahi wa Magharibi kuhusiana na Halab sasa umegonga mwamba na hivyo kudidimiza matarajio yake  kuhusiana na matukio ya Syria. Marekani na washirika wake wanaituhumu serikali ya Syria kuwa ndiyo iliyozua mgogoro wa hivi sasa wa nchi hiyo katika hali ambayo ukweli wa mambo ni kuwa ni wao na vibaraka wao wa kigaidi ndio waliovura uthabiti wa nchi hiyo. Kwa vyovyote vile ushindi wa serikali na wanamapambano nchini Syria huko Halab umewashangaza magaidi na mabwana zao wa Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu kiasi kwamba sasa wameanzisha wimbi kubwa la propaganda kwa ajili ya kuchafua na kufunika ushindi huo.

Kwa upande wa pili serikali zinazofadhili ugaidi zimachukua mkondo mpya wa kuwaunga mkono magaidi walioshindwa mjini Halab kwa kuimarisha operesheni za magaidi hao katika maeneo mengine ya Syria ili kudumisha harakati zao nchini humo.

Askari wa Syria wakiwa katika moja ya operesheni za kuukomboa mji wa Aleppo

Serikali hizo zinaeneza propaganda na uchochezi eti kwamba mabavu yametumiwa na askari wa serikali katika ukombozi wa Halab katika hali ambayo ni magaidi ndio wametekleleza jinai na vitendo vya kikatili katika kipindi chote walichokuwa wameuteka mji huo na kuukalia kwa mabavu, na serikali hizo za Magharibi na vibaraka wao wa nchi za Kiarabu kukaa kimya na kutosema lolote kuhusiana na jinai hizo. Kuendelea kushindwa magaidi huko Syria na nchi nyingine kama vile Iraq na Libya kunabainisha wazi kwamba magaidi na wafadhili wao, licha ya kutekeleza mbinu za ujanja na hila lakini wameshindwa kufunika kushindwa kwao katika nchi hizo na hasa katika mji wa Halab huko Syria.