Ukiukwaji haki za binadamu Bahrain sasa walalamikiwa Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i30516-ukiukwaji_haki_za_binadamu_bahrain_sasa_walalamikiwa_ulaya
Kutokana na kuendelea ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa kiimla wa Aal Khalifa nchini Bahrain, Bunge la Ulaya sasa limevunja kimya chake na kulalamikia hatua hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2017 23:52 UTC
  • Ukiukwaji haki za binadamu Bahrain sasa walalamikiwa Ulaya

Kutokana na kuendelea ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa kiimla wa Aal Khalifa nchini Bahrain, Bunge la Ulaya sasa limevunja kimya chake na kulalamikia hatua hiyo.

Zaidi ya wabunge 300 wa bunge hilo wameandika barua na kumkabidhi Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya wakimtaka afuatilie suala hilo. Katika barua hiyo wabunge hao wameeleza wasiwasi wao mkubwa kuhusu hali mbaya ya haki za binadamu nchini Bahrain.

Wabunge hao aidha wameutaka utawala wa Aal Khalifa umwachilie huru mara moja Nabil Rajab, mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu nchini Bahrain. Aidha wametaka waachiliwe huru wanaharakati wote wa kisiasa wanaoshikiliwa katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Hivi sasa inaonekana kuwa jamii ya kimataifa imechoshwa na ukiukwaji na ukandamizaji unaofamywa na ukoo wa Aal Khalifa dhidi ya Wabahrain.

Polisi nchini Bahrain wanatumia nguvu ziada kukabiliana na wananchi wanaoandamana

Mapema mwezi huu wa Juni, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad  al-Hussein  alitoa wito wa kufanyika uchunguzi huru baada ya wanajeshi wa Bahrain kuivamia nyumba ya Ayatullah Sheikh Isa Qassim katika eneo la Diraz, kaskazini mwa Manama. Katika hujuma hiyo ya mwishoni mwa mwezi Aprili, vijana watano waliokuwa wakimtetea mwanazuoni huyo wa Kiislamu waliuawa kwa kupigwa risasi na jeshi la utawala wa Aal Khalifa. Al-Hussein aidha alieleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu kukamatwa wapinzani Bahrain.

Pamoja na ukosoaji huo wa taasisi muhimu za kimataifa, lakini serikali za nchi za Magharibi hazijaonyesha msimamo wa kuchukua hatua kali kukabiliana na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Bahrain, nchi ambayo ni muitifaki mkubwa wa Uingereza na Marekani. Hata baada ya taasisi sita muhimu za haki za binadamu kutoa taarifa ya pamoja hivi karibuni zikilaani mateso na kushikiliwa wafungwa wa kisiasa huko Bahrain sambamba na kuitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua kukabiliana na hali hiyo, lakini madola ya Magharibi yalipuuza kabisa ombi hilo.

Wakati huo huo tunashuhudia baadhi ya nchi za Ulaya hasa Uingereza, Ujerumani na Marekani zikiendeleza kuiuzia serikali ya Bahrain silaha na zana za kukabiliana na waandamanaji na hivyo kuunga mkono moja kwa moja ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa ukoo wa Aal Khalifa.

Nabil Rajab, mtetezi wa haki za binadamu Bahrain

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kuuziwa Bahrain silaha za nchi za Magharibi ni jambo linalokiuka misingi ya haki za binadamu.

Tunaweza kusema kuwa, barua wa wabunge 300 wa Bunge la Umoja wa Ulaya wakilalamikia hali ya mambo nchini Bahrain ni kati ya sera za kindumakuwili za  nchi za Magharibi kuhusu haki za binadamu. Katika upande mmoja tunaona bunge likidai kuwa  linaulaani utawala wa Aal Khalifa na kwa upande wa pili nchi hizo za Ulaya zinashirikiana na kuimarisha uhusiano na utawala  wa Bahrain unaoendelea kuwakandamiza wananchi.