Kuendelea kushikiliwa wanaharakati wa kisiasa nchini Bahrain
Katika mwendelezo wa kuwakandamiza wapinzani nchini Bahrain, mahakama ya nchi hiyo imetoa hukumu ya kifungo cha miaka miwili jela dhidi ya Nabil Rajab, Mkuu wa Kituo cha Haki za Binadamu nchini Bahrain kwa tuhuma za kueneza habari za uongo na uvumi kuhusiana na hali ya ndani ya nchi hiyo.
Nabil Rajab, mwanaharakati wa haki za binadamu wa Bahrain alitiwa mbaroni kutokana na kukosoa hatua za ukandamizaji za utawala wa nchi hiyo wa Aal Khalifa na kushiriki Bahrain katika muungano wa Saudia dhidi ya Yemen. Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Wrights Watch mara kadhaa limetoa wito wa kuachiliwa huru mwanaharakati huyo, lakini hadi sasa serikali ya Manama imekataa kutekeleza takwa hilo.
Ripoti mbalimbali kutoka Bahrain zinaonyesha kuwa, utawala wa Aal Khalifa ungali unaendelea kufanya ukandamizaji na kutumia mkono wa chuma dhidi ya wanaharakati wa kisiasa huku ukiwatupa jela wapinzani wa nchi hiyo kwa kutumia vizingizio mbalimbali. Kwa hakika matukio ya Bahrain yanaonyesha kwamba, ukandamizaji umeshadidi nchini humo na hatua ya utawala wa Manama ya kukithirisha vitendo vya kuwakamata wanaharakati wa kisiasa na wa haki za binadamu, zimeifanya nchi hiyo itawaliwe na anga ya mbinyo wa kisiasa.
Aidha utawala wa Bahrain umeongeza kasi ya kutoa hukumu za vifungo mbalimbali jela dhidi ya wapinzani ambapo harakati zake hizo za kuwatupa jela wapinzani zimeigeuza nchi hiyo na kuifanya kuwa moja ya nchi zenye wafungwa wengi wa kisiasa kwa mujibu wa idadi ya wakazi wake.
Hapana shaka kuwa, jambo hilo linazidi kuweka wazi utambulisho wa utawala huo ambao ni kutumia mabavu na ukandamizaji dhidi ya raia. Edward Kerrigan, mtaalamu wa masuala ya kimataifa wa Canada anasema:
"Utawala wa Bahrain ungali unaendelea kuamiliana vibaya na wapinzani. utawala huo unatekeleza sheria nyingi dhidi ya wapinzani wake na yeyote anayejitokeza na kuonyesha kutoridhishwa na utendaji wa utawala wa Manama au asimame na kutaka kuleta mabadiliko, basi hatua yake hiyo huhesabiwa kuwa ni ya kigaidi. Na katika mazingira kama hayo, wananchi wa Bahrain hawawezi kupaza sauti yoyote ile ya malalamiko na kupigania demokrasia."
Ukweli ni kwamba, wananchi wa Bahrain chini ya utawala wa ukoo wa Aal Khalifa hawana haki yoyote na utawala huo hausiti kuchukua hatua yuoyote ile ya kuwapokonya wananchi hao haki ndogo kabisa kama ya kisiasa, kijamii na kiraia.
"Catherine Shakdam, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti Mashariki ya Kati cha London Uingereza amesisitiza kuwa: Ukandamizaji wa wapinzani nchini Bahrain ni sehemu ya mpango mkubwa zaidi wa utawala wa Manama wa kupinga matakwa ya umma kwa ajili ya demokrasia.
Aidha anasema: Ukweli wa mambo ni kuwa, utawala wa Bahrain hauna nia kabisa ya kuruhusu demokrasia katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Hii ni katika hali ambayo, licha ya hayo yote utawala wa Bahrain umeendelea kupata himaya na uungaji mkono wa madola ya Magharibi. Hapana shaka kuwa, jambo hilo ndilo linaloupa kiburi utawala huo cha kuendeleza siasa zake zilizo dhidi ya ubinadamu.
Ukweli wa mambo ni kuwa, moja ya matatizo na malalamiko ya wananchi wa Bahrain kwa utawala wa Aal Khalifa ni muundo wa kisiasa unaotawala nchini humo ambao una misingi ya udikteta na kuwafarakanisha wananchi.
Kuhodhiwa madaraka na utajiri wa nchi na familia moja tu ya Aal khalifa huku wananchi wakiwekewa mbinyo na ukandamizaji mkubwa, ni moja ya sababu zilizopelekea subira ya wananchi wa nchi hiyo kufikia kikomo na kuamua kuanzisha harakati za kupigania uhuru.
Tangu Februari 14 mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia vuguvugu la mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala wa Aal Khalifa wa nchi hiyo. Wananchi hao wanataka kuweko uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali ambayo imechaguliwa na wananchi wenyewe. Hatua zote za utawala huo za kuzima vuguvugu hilo hadi sasa hazijafanikiwa.
Akthari ya wananchi wa Bahrain, Mashia kwa Masuni wote wanalalamikia muundo wa kisiasa wa nchi hiyo. Mahudhurioa makubwa ya wananchi wa kawaida na makundi ya kisiasa ya Waislamu wa madhehebu ya Kisuni katika kuupinga utawala wa Manama ni ithbati tosha kwamba, vuguvugu la mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo halina hisia za kimakundi kinyume na madai ya watawala wa nchi hiyo.