Ombi la Russia la kutaka kufutwa haraka vikwazo dhidi ya Syria
Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia jana Jumatano akihutubia waandishi wa habari akiwa ameandamana na waziri mwenzake wa Jordan Ayman Safadi mjini Moscow, alitangaza kuwa, vikwazo vyote dhidi ya Syria vinapaswa kuondolewa na Wasyria wasaidiwe kurejea katika nchi yao.
Lavrov akijibu baadhi ya uvumi kuhusu kuondoka wanajeshi wa Iran nchini Syria alisema ni kutozingatia uhalisia wa mambo kutaraji kuwa Iran itaondoka Syria na isiwe na nafasi katika eneo.
Sisitizo la Russia la kuondolewa haraka vikwazo dhidi ya Syria linatokana na kuzingatia matukio ya hivi karibuni nchini humo, yaani kushindwa mutawalia makundi ya kigaidi na kufanikiwa serikali halali ya Syria kuchukua udhibidi wa maeneo mengi ya nchi hiyo.
Aidha kwa kuendelea hali ya hivi sasa ya kutimuliwa magaidi, suala la dharura ni kurejea wakimbizi Waysira katika miji na vijiji vyao ili hali ya kawaida irejee katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita vya miaka kadhaa. Umoja wa Mataifa pia unasisitiza udharura wa kuondolewa vikwazo ilivyowekewa Syria. Idriss Jazairy Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa anasema vikwazo vya upande mmoja vya nchi za Magharibi vimekuwa na taathira hasi nchini Syria.
Jazairy amependekeza kuundwe kundi la kiufundi ambalo litawashirikisha wawakilishi wa pande zote husika katika vikwazo dhidi ya Syria ili kufanyike mazungumzo ya kupunguza vikwazo hivyo na kwa njia hiyo misaada ya kibinaadamu iwafikia Wasyria.
Madola ya Magharibi yaani nchi za Ulaya na Marekani, tokea mwaka 2011 wakati machafuko yalipoanza Syria na kisha vita vya ndani kuibuka nchini humo, yamekuwa yakifanya juu chini kuidhoofisha serikali ya kisheria nchini humo inayoongozwa na Rais Bashar Al Assad. Aidha madola hayo ya Magharibi yamekuwa yakiyapa nguvu makundi ya kigaidi sambamba na kuweka vikwazo vingi dhidi ya Syria.
Katika hatua ya hivi karibuni ya vikwazo dhidi ya Syria, mnamo Mei 28 2018, Umoja wa Ulaya ulitangaza kurefusha kwa mwaka mmoja zaidi vikwazo dhidi ya Syria. Marekani nayo pia inaendelreza vikwazo dhidi ya Syria.
Kuendelezwa vikwazo vya magharibi dhidi ya Syria kunamaanisha kuwa nchi za Magharibi zina mtazamo hasi kuhusu mchakato wa utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Syria.
Mgogoro huo ulianza mwaka 2011 wakati Marekani ikishirikiana na baadhi ya nchi za Ulaya na Kiarabu zilianza kuunga mkono makundi ya kigaidi nchini Syria. Nchi hizo, zikiwemo Ufaransa na Uingereza zilianzisha muungano wa Kiarabu na Kimagharibi kwa lengo la kuiangusha serikali halali ya Syria. Muungano huo ulitoa msaada wa pande zote kwa magaidi na makundi ya wabeba silaha kwa dhana potovu kuwa makundi hayo yangeweza kuiangusha serikali ya Rais Bashar al Assad. Lengo kuu la sera hiyo lilikuwa ni kutoa pigo kwa Syria ambayo ni kitovu cha mhimili wa muqawama au mapambano dhidi ya Uzayuni katika eneo. Muungano huo ulitaraji kuwa kuangushwa serikali ya Syria kungepelekea kusambaratika mhimili wa muqawama katika eneo. Hata hivyo muungano huo umegonga mwamba katika lengo lake la kuanzisha vita vya ndani nchini Syria.
Hivi sasa mlingano wa nguvu nchini Syria umebadilika kikamilifu kwa maslahi ya serikali halali ya nchi hiyo na waitifaki wake.
Ni kwa msingi huo ndio Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov akaunga mkono wazi wazi kuendelea kubakia Iran kijeshi nchini Syria kinyume cha matakwa ya madola ya Magharibi na utawala haramu wa Israel
Kama alivyosema Aron Lund, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Sweden, Rais Bashar al Assad amefanikiwa kistratijia kuwashinda maadui ambao walikuwa wanalenga kumuondoa madarakani.
Hivi sasa makundi ya kigaidi nchini Syria yamedhoofika kikamilifu na serikali ya Syria, ikishirkiana na waitifaki wake yaani, Russia, Iran na Harakati ya Hizbullah, wanalenga kukamilisha ushindi huo kwa kuwatimua kikamilifu magaidi katika maeneo yote ya nchi hiyo hasa mkoani Daraa. Hata nchi za Magharibi zikiendelea kuiwekea Syria vikwazo, haziwezi kuteteresha azma ya serikali ya Rais Assad katika kuwaangamiza kikamilifu magaidi nchini humo.