Malengo mawili ya ziara ya Mahmoud Abbas nchini Misri
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i100610-malengo_mawili_ya_ziara_ya_mahmoud_abbas_nchini_misri
Mahmoud Abbas, mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina (PA), ambaye alisafiri kwenda Misri kushiriki katika kikao cha makatibu wakuu wa makundi ya Palestina, alikutana na Rais Abdel Fattae el Sisi wa nchi hiyo na pia mkuu wa idara ya kijasusi wa nchi hiyo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 02, 2023 22:57 UTC
  • Malengo mawili ya ziara ya Mahmoud Abbas nchini Misri

Mahmoud Abbas, mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina (PA), ambaye alisafiri kwenda Misri kushiriki katika kikao cha makatibu wakuu wa makundi ya Palestina, alikutana na Rais Abdel Fattae el Sisi wa nchi hiyo na pia mkuu wa idara ya kijasusi wa nchi hiyo.

Ziara ya Mahmoud Abbas nchini Misri ni muhimu kutokana na nukta mbili.

Kwanza ni kuwa, mikutano ya Abbas na viongozi wa Misri imekuwa na umuhimu mkubwa kwa sababu ya nafasi ya Misri katika maetukio ya ndani ya Palestina na pia katika mgogoro kati ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel. Hadi sasa, Misri imekuwa mahali pa kukutana viongozi mbalimbali wa Palestina na wapatanishi baina yao, na pia mara kadhaa imekuwa mpatanishi baina ya Wazayuni na Wapalestina. Kwa kuzingatia kuongezeka mvutano na mzozo kati ya Wapalestina na Wazayuni, mkutano wa Mahmoud Abbas na viongozi wa Misri inaweza kwa mara nyingine tena kutoa fursa kwa Cairo kuwa mpatanishi katika mgogoro uliopo.

Suala la pili la umuhimu wa ziara ya Mahmoud Abbas mjini Cairo ni kuhusiana na kikao cha makatibu wakuu wa makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina kilichofanyika Cairo chini ya usimamizi wa Mahmoud Abbas.

Inafaa kuashiria hapa kuwa Mahmoud Abbas, Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, aliwaalika makatibu wakuu wa makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina kushiriki katika mkutano huo nchini Misri. Hata hivyo, mkutano huo uliofanyika Julai  ulisusiwa na makundi matatu, ikiwa ni pamoja na Harakati ya Jihad Islami, Harakati ya Wananchi Kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina na Harakati ya Radi.

Sababu kuu ya kutoshiriki makundi hayo katika kikao cha hivi karibuni cha Misri ni kuhusiana na hatua ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kukataa kuwaachilia wafungwa wa kisiasa. Hivi karibuni, badala ya kuyapongeza makundi ya muqawama na mapambano ya Palestina kutokana na mapambano yao shupavu dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel, Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetia mbaroni idadi kubwa ya wanachama wa makundi hayo jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa vikali na makundi ya muqawama ya Palestina.

Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniya  (kushoto) na Mahmoud Abbas

Kuhusiana na suala hilo, Khizr Habib, mmoja wa viongozi wa harakati ya Jihad Islami amesema: "Harakati ya Jihad Islami inaibebesha lawama Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa kushindwa kufanyika mkutano huu. Kwa sababu kabla ya kuanza kwake, Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilisisitiza juu ya kuendelea kutiwa mbaroni wapiganaji wa muqawama na wanasiasa wa makundi ya muqawama." Amesema kundi hilo halikushiriki katika mkutano wa makatibu wakuu wa makundi ya muqawama nchini Misri kutokana na upinzani wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wa kuachiliwa wafungwa wa kisiasa.

Levi al-Qariyoti, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Wananchi Kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina, pia ameshikilia msimamo huo huo na kusema ili kufanikisha mkutano wa Cairo kwanza ilikuwa ni lazima  kuachiliwa wafungwa wa kisiasa na wapiganaji waliofungwa katika jela za Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Ameongeza kuwa: Kwa kuzingatia kuwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekataa kuwaachilia huru wafungwa, Harakati ya Wananchi Kwa Ajili ya Ukombozi wa Palestina pia iliamua kutoshiriki katika mkutano wa Cairo.

Kutoshiriki baadhi ya makundi ya Wapalestina katika kikao hicho cha Misri na ukosoaji wa a Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuhusu Jihad Islami kunaashiria kuwa kikao cha Misri hakikuweza kuimarisha nafasi dhaifu na inayotetereka ya Mahmoud Abbas huko Palestina, ukiwemo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.