Walowezi wa Kizayuni waliwashambulia Wapalestina mara 900 Julai
Kamisheni ya mapambano ya Palestina imesema katika ripoti yake mpya kuwa, vikosi vya utawala haramu wa Israel pamoja na walowezi wa Kizayuni waliwashambulia Wapalestina na maeneo yao matakatifu karibu mara 900 mwezi uliopita wa Julai.
Kamisheni ya Ukuta wa Palestina na Mapambano dhidi ya Vitongoji vya Walowezi wa Kizayuni imesema Wazayuni waliwashambulia moja kwa moja Wapalestina, kupora mali zao, kushambulia vijiji, kuchoma nyumba na kung'oa miti katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu.
Shirika la habari la WAFA limeripoti habari hiyo leo Jumapili na kueleza kuwa, aghalabu ya mashambulizi hayo 897 yalitokea katika mji mtukufu wa Quds uliosajili kesi 148, Nablus 140 na al-Khalil matukio 113.
Tume hiyo imesema Wazayuni walifanya mashambulizi 202 dhidi ya maeneo mbalimbali katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu, hasa Nablus na Ramallah.
Wakati huohuo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema vikosi vya utawala haramu wa Israel pamoja na walowezi wa Kizayuni waliyashambulia Wapalestina na maeneo yao matakatifu mara 591 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu.
Jens Laerke, Msemaji wa taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa alisema hayo jana Jumamosi mjini Geneva na kuongeza kuwa, matukio hayo ni sawa na wastani wa hujuma 99 kila mwezi, na hilo linaashiria ongezeko la asilimia 39 ikilinganishwa na matukio yaliyosajiliwa kila mwezi mwaka uliopita 2022.