Ripoti: Saudia inairubuni Palestina kwa fedha ili ikubali uhusiano na Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i101650-ripoti_saudia_inairubuni_palestina_kwa_fedha_ili_ikubali_uhusiano_na_israel
Maafisa wa Saudi Arabia wameripotiwa wakisema kuwa, Riyadh ipo tayari kuanza tena kuipa Mamlaka ya Ndani ya Palestina msaada wa kifedha, mkabala wa kupata uungaji mkono wa Ramallah katika juhudi zake za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 30, 2023 04:44 UTC
  • Ripoti: Saudia inairubuni Palestina kwa fedha ili ikubali uhusiano na Israel

Maafisa wa Saudi Arabia wameripotiwa wakisema kuwa, Riyadh ipo tayari kuanza tena kuipa Mamlaka ya Ndani ya Palestina msaada wa kifedha, mkabala wa kupata uungaji mkono wa Ramallah katika juhudi zake za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Gazeti la Wall Street Journal limeripoti hayo jana Jumanne, ambapo limenukuu maafisa ambao majina yao hayakutajwa wa Saudia wakisema kuwa, mara ya kwanza Mrithi wa Ufalme wa Saudia, Mohammed bin Salman kutoa pendekezo hilo ilikuwa ni Aprili mwaka huu, wakati wa safari ya Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas mjini Jeddah.

Katika mazungumzo hayo, Bin Salman alisema kuwa Riyadh ipo tayari kuendelea kuipa misaada ya kifedha Palestina, na kwamba makubaliano yoyote ya kuanzisha uhusiano na Israel, hayataathiri jitihada za kuundwa taifa huru la Palestina.

Ripoti ya Wall Street Journal imedokeza kuwa, Saudia inatumai kuwa, Abbas kubariki uhusiano na Tel Aviv kutawanyamazisha wakosoaji wa watawala wa Riyadh wanaotuhumiwa kuipa mkono kadhia ya Palestina.

Saudia imeipa Mamlaka ya Ndani ya Palestina misaada yenye thamani ya dola bilioni 5 tokea mwaka 1948, lakini ilianza kupunguza msaada huo mwaka 2016, kutoka dola milioni 174 kwa mwaka mnamo mwaka 2019, hadi sifuri  2021.

Licha ya kuwa hadi sasa hakuna uhusiano rasmi baina ya Israel na Saudi Arabia, lakini pande hizo mbili hususan kuanzia mwaka 2020 zimechukua hatua katika mkondo wa kupanua wigo wa ushirikiano wao. 

Serikali ya Riyadh mwaka jana ilifungua anga yake kwa ajili ya ndege za Israel, na juzi Jumatatu, irihusu ndege ya Air Sychelles iliyokuwa imebeba abiria 128 wa utawala huo pandikizi kuelekea Tel Aviv, kutua mjini Jeddah eti baada ya kupatwa na hitilafu za kiufundi.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel hapo jana alitoa taarifa ya kuishukuru Saudia kwa kuruhusu ndege hiyo itue kwa dharura mjini Jeddah, na kusema kuwa kitendo hicho kimeonyesha ujirani mwema.