Shirika: Israel inaua watoto 100 wa Kipalestina kila siku
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i103636-shirika_israel_inaua_watoto_100_wa_kipalestina_kila_siku
Shirika moja la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini Geneva Uswisi limesema kwa wastani utawala haramu wa Israel unaua shahidi watoto 100 wa Kipalestina katika kila saa 24 katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 18, 2023 08:55 UTC
  • Shirika: Israel inaua watoto 100 wa Kipalestina kila siku

Shirika moja la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini Geneva Uswisi limesema kwa wastani utawala haramu wa Israel unaua shahidi watoto 100 wa Kipalestina katika kila saa 24 katika Ukanda wa Gaza.

Shirika hilo la Euro-Mediterranean Human Rights Observatory limesema katika ripoti kuwa, limenakili vifo 1,046 vya watoto wa Kipalestina kufikia Oktoba 16, mbali na majeruhi 3,250, wakiwemo watoto 1,240 wanaohitaji huduma maalum za matibabu.

Aidha shirika hilo limesema watoto wasiopungua 167 wa Palestina wamenasa kwenye vifusi vya majengo ya makazi ya raia yaliyolengwa na hujuma za anga za utawala haramu wa Israel huko Gaza.

Shirika la Euro-Mediterranean Human Rights Observatory lenye makao yake mjini Geneva limeongeza kuwa, watoto ndio wahanga na walengwa wa kwanza wa 'umwagaji damu' unaoendelea dhidi ya Wapalestina Gaza.

Watoto wa Kipalestina,wahanga wakuu wa jinai za Israel huko Gaza

Viongozi wa nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa yameendelea kulaani mauaji ya kinyama yanayofanywa na jeshi la Israel dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza. 

Kwa mujibu wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), kwa akali watoto 447 wa Kipalestina walikuwa wameuawa hadi kufikia Oktoba 14 huko Gaza kufuatia mashambulio ya jeshi la Israel dhidi ya eneo hilo.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ilisema juzi Jumatatu kuwa, nchi zinazounga mkono uvamizi wa Israel katika hujuma yake inayoendelea dhidi ya Ukanda wa Gaza zinahusika katika mauaji ya watoto, wanawake na raia.