Pyongyang: Israel imefanya jinai ya kivita kwa kushambulia hospitali Gaza
Korea Kaskazini imelaani vikali shambulio la anga lililofanywa na jeshi la utawala haramu wa Israel dhidi ya Hospitali ya Al Ahli Arab katika Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 17 na kuua mamia ya wananchi wa Paalestina.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini imesema hayo katika taarifa iliyorushwa hewani na shirika rasmi la habari la nchi hiyo KCNA na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni umefanya jinai za kivita dhidi ya Wapalestina wa Gaza, huku ukikingiwa kifua na Marekani.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa inapasa kuchukua hatua za dharura za kukabiliana na jinai hizo za Wazayuni dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza ambao umezingirwa.
Jamii ya kimataifa ililaani shambulizi hilo la Oktoba 17 lililoua Wapalestina wasiopungua 500 katika Ukanda wa Gaza, na kutaka ulinzi wa haraka kwa raia na vituo vya afya katika eneo hilo la Palestina.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini imebainisha kuwa, Marekani ni mshirika katika jinai za kutisha za Israel huko Ukanda wa Gaza kutokana na uungaji mkono wake wa hali na mali kwa utawala huo unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Pyongyang imeeleza kuwa: Marekani imeipa Israel taa ya kijani iendelee kuwaua kwa umati Wapalestina bila wasi wasi wowote. Washington imeipa Israel misaada ya kijeshi na silaha, ikiwemo kutuma manowari za kubeba ndege za kivita Mashariki ya Kati.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini imeongeza kuwa, Marekani ndiyo iliyohusika na vita vya Israel na HAMAS, na kusisitiza kuwa Washington ndiyo inayofaa kubebeshwa dhima ya mgogoro huo.
Idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi tangu utawala haramu wa Israel ulipoanza kufanya mashambulio ya anga katika Ukanda wa Gaza Oktoba 7 imepindukia 7,000, huku makumi ya maelfu ya wengine wakiwa wamejeruhiwa au kutoweka.