Kata'ib Hizbullah: Ziara ya Blinken nchini Iraq haikubaliki
(last modified Mon, 06 Nov 2023 03:00:19 GMT )
Nov 06, 2023 03:00 UTC
  • Kata'ib Hizbullah: Ziara ya Blinken nchini Iraq haikubaliki

Harakati ya Muqawama ya Kata'ib Hizbullah ya Iraq imetishia kushadidisha hali ya taharuki iwapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken atafanya safari ya kuitembelea Baghdad.

Abu Ali al-Askari, Kiongozi wa Ofisi ya Usalama ya Kata'ib Hizbullah amesema safari ya Blinken nchini Iraq, ambaye amemtaja kuwa waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni, haikubaliki.

Shirika la habari la SAMA limemnukuu al-Askari akisema kuwa: Iwapo (Blinken) atakuja (Iraq), tutamkabili kwa hatua ambazo hazijawahi kushuhudiwa.

Amesema Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na wa eneo ni washirika wa jinai za kutisha zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Wapalestina karibu 10,000 wameuawa shahidi katika hujuma za Israel Gaza.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Harakati ya Muqawama ya Kata'ib Hizbullah ameeleza kuwa, kundi hilo la mapambano ya Kiislamu nchini Iraq litachukua hatua za kuhitimisha maslahi ya Marekani si tu katika nchi hiyo ya Kiarabu, bali katika eneo zima la Asia Magharibi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani (kushoto) na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani, Palestina

Kauli ya Kiongozi wa Ofisi ya Usalama ya Kata'ib Hizbullah ya Iraq imekuja baada ya vyombo vya habari vya Iraq kutangaza kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken alitarajiwa kuwasili Baghdad Jumapili.

Aidha haya yanajiri siku chache baada ya vituo vya kijeshi vya Marekani kushambuliwa katika hujuma za ndege zisizo na rubani (droni) katika eneo la Kurdistan la kaskazini mwa Iraq na katika mkoa wa Hasaka, mashariki mwa Syria.

Tags