Iran: Marekani inaipa Israel silaha zilizopigwa marufuku kimataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameikosoa vikali Marekani kwa kuipa Israel silaha zilizoharamishwa kimataifa kama vile mabomu ya fosforasi ili utawala huo wa Kizayuni utumie silaha hizo dhidi ya wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo Jumatano mjini Geneva, Uswisi katika mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa: Kwa masikitiko, tunashuhudia hali ambayo, Wamarekani wanatuma kila aina ya silaha yakiwemo mabomu yaliyopigwa marufuku ya fosforasi huko Tel Aviv kutokea Cyprus au moja kwa moja kutoka kwenye kambi zao (za kijeshi) katika eneo (la Asia Magharibi).
Amesema mabomu hayo yaliyopigwa marufuku kimataifa ya Marekani yanadondoshewa na jeshi la utawala haramu wa Israel huko Gaza dhidi wananchi madhulumu na shupavu wa Palestina.
Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, jinai zinazofanywa na Wazayuni kwa uungaji mkono wa hali na mali wa Marekani katika eneo hilo lililozingira ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Amesema Marekani inabeba dhima ya kuendelea uvamizi na hujuma za kinyama dhidi ya Wapalestina wa Gaza, na kwamba kuna haja ya kufanyika jitihada za kusimamisha vita hivyo mara moja.
Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameongeza kuwa, akiwa ziarani Geneva, atafanya mazungumzo na maafisa wa Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) kujadili suala la kutumwa shehena za misaada ya Jamhuri ya Kiislamu kwa wakazi wa Gaza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vikali unafiki na undumakuwili wa Washington kwa kufumbia macho na hata kushajiisha mashambulizi ya kikatili ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Takwimu za karibuni zinaonyesha kuwa, idadi ya mashahidi wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza tokea Oktoba 7 hadi sasa inakaribia watu 12,000, na waliojeruhiwa ni zaidi ya 29,000.