Jihad Islami: Israel imeshindwa kuusambaratisha muqawama
Mjumbe wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina mjini Tehran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel haujafikia hata moja ya malengo yake ya kuanzisha mashambulizi ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, hasa azma ya utawala huo ya kuusambaratisha mrengo wa muqawama.
Nasser Abu-Sharif amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la ISNA na kuongeza kuwa: Lengo kuu la utawala wa Kizayuni lilikuwa ni kuvisambaratisha vikosi vya muqawama, lakini licha ya ukatili na jinai ulizozitekeleza kwa uungaji mkono wa madola ya kiistikbari, haujaweza kuambulia chochote."
Ameeleza bayana kuwa, uvamizi wa Israel ulioanza Oktoba 7 dhidi ya Gaza umeusababishia utawala wa Kizayuni hasara kubwa zikiwemo za kiuchumi, na hivi sasa utawala huo pandikizi umelemaa kikamilifu.
Abu-Sharif amebainisha kuwa, mashambulizi ya kikatili ya Israel yamefichua dhati ya ukatili na sura halisi ya nchi za Magharibi kwa namna zinavyouunga mkono utawala huo unaoua watoto na wanawake wa Kipalestina.
Mjumbe wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina hapa nchini Iran ameeleza kuwa, "Magharibi haiheshimu sheria za kimataifa, uhuru na kanuni za kimaadili."
Kwengineko kwenye mahojiano hayo na ISNA, afisa huyo wa ngazi ya wa Harakati ya Muqawama ya Jihad Islami ya Palestina amepongeza na kusifu msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kadhia ya Gaza.
Aidha amepongeza matamshi ya Rais Ebrahim Raisi wa Iran katika mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) uliofanyika mapema mwezi huu mjini Riyadh, Saudi Arabia.
Sayyid Raisi alisisitiza katika kikao hicho kwamba: Kadhia ya Gaza ni makabiliano baina ya mhimili wa sharafu na mhimili wa uovu, na kila mtu anapaswa abainishe yuko upande gani.