Imarati yawataka raia wake wasivae kanzu, buibui wakiwa nje ya nchi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i10576-imarati_yawataka_raia_wake_wasivae_kanzu_buibui_wakiwa_nje_ya_nchi
Imarati (UAE) imewataka raia wake wajiepushe kuvaa kanzu na buibui wakiwa nje ya nchi ili wasifananishwe na wafuasi wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 04, 2016 09:53 UTC
  • Imarati yawataka raia wake wasivae kanzu, buibui wakiwa nje ya nchi

Imarati (UAE) imewataka raia wake wajiepushe kuvaa kanzu na buibui wakiwa nje ya nchi ili wasifananishwe na wafuasi wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh

Katika ujumbe uliotumwa kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, Wiizara ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), imesema kuwa, kwa usalama wao, raia wanaosafiri nje ya nchi wanatakiwa kutovaa mavazi rasmi ya kitaifa ambayo ni kanzu na hagali kwa wanaume na buibui na mtandio kwa wanawake.

Taarifa hiyo imekuja wiki moja baada ya mfanya biashara mmoja wa Imarati kukamatwa akiwa amevalia kanzu na hagali huko Ohio Marekani baada ya mfanyakazi wa hoteli kumshuku kuwa ni gaidi mkufurushaji.

Mfanyakazi huyo wa hoteli aliwapigia simu polisi baada ya kumuona raia huyo wa Imarati akiwa amevalia vazi hilo huku akizungumza kwa lugha ya Kiarabu kwa simu yake ya mkononi. Aliachiliwa baada ya polisi kubaini kuwa alikuwa ni mfanyabiashara wa kawaida.

Taarifa hiyo pia imewataka raia wa kike Imarati kutovaa nikabu kwani imepigwa marafuku kuvaliwa hadharani katika baadhi ya miji ya Ulaya.

Kumeshuhudiwa ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu Ulaya na Marekani kutokana na ongezeko la wakimbizi Waislamu na pia ukatili wa magaidi wa kundi la ISIS huko Iraq na Syria.