Katika siku ya 80 ya uvamizi ulioanzishwa na utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya Gaza, maafa makubwa linayopata jeshi la utawala huo dhalimu katika vita vya ardhini pamoja na mashambulio makali na makubwa linayofanya jeshi hilo katika maeneo mbalimbali ya Gaza, ni matukio ambayo yangali yanaendelea kushuhudiwa katika eneo hilo.
Changamoto zinazoikabili Israel na Marekani za kuendeleza vita vya Gaza
Dec 25, 2023 07:03 UTC
Katika siku ya 80 ya uvamizi ulioanzishwa na utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya Gaza, maafa makubwa linayopata jeshi la utawala huo dhalimu katika vita vya ardhini pamoja na mashambulio makali na makubwa linayofanya jeshi hilo katika maeneo mbalimbali ya Gaza, ni matukio ambayo yangali yanaendelea kushuhudiwa katika eneo hilo.
Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kuwa mapigano, makali kati ya Muqawama wa Palestina na wanajeshi wa utawala ghasibu wa Kizayuni yangali yanaendelea huko Jabaliya al-Balad kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
Kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, askari wa jeshi vamizi la Kizayuni wamekuwa wakijaribu kupenya ndani ya Jabalia sambamba na mashambulio ya mtawalia ya angani na ya mizinga linalofanya jeshi hilo, lakini hadi sasa wamekabiliwa na upinzani mkali wa makundi ya Muqawama wa Palestina.
Sambamba na kushadidi mashambulizi ya anga na mizinga ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika eneo zima la Ukanda wa Gaza, wapiganaji wa Muqawama wa Palestina walioko kaskazini ya Gaza na wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, wanaendelea kuwashambulia askari wa jeshi la Israel na kutoa vipigo vikali kwa wazayuni hao.
Netanyahu anayeshupalia kuendeleza vita kwa gharama yoyote
Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa, utawala wa Kizayuni unajiandaa hatua kwa hatua kulegeza msimamo mbele ya matakwa ya Muqawama wa Palestina na kukaribia zaidi kuyakubali masharti na matakwa ya Hamas.
Chaneli ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imemnukuu afisa mmoja wa ngazi za juu wa Israel akisema, "tuko kwenye marhala ya kusubiri kuwadia siku muhimu sana za ubadilishanaji mpya wa mateka."
Siku ya Jumamosi, maelfu ya wakazi wa ardhi zinazokakliwa kwa mabavu walifanya maandamano makubwa mjini Tel Aviv. Waandamanaji hao waliitaka serikali ya Kizayuni ifikie makubaliano na Hamas kwa ajili ya kuachiliwa mateka wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Gaza.
Vilevile katika maandamano hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Habima mjini Tel Aviv, waandamanaji walimtaka Waziri Mkuu wa utawala huo wa Kizayuni Benjamin Netanyahu ajiuzulu.
Askari mstaafu wa Kizayuni anayeamini kuwa Isarel haiwezi kuishinda HAMAS
Baada ya kuanzisha operesheni za kijeshi huko Gaza, utawala ghasibu wa Israel umekabiliwa na kibarua kigumu cha kuzituliza fikra za waliowengi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina la Israel. Sambamba na utawala huo kusisitiza kwamba unafanya juhudi za kuwakomboa mateka wanaoshikiliwa na Hamas, ungali unataka kupanua wigo wa operesheni zake za kijeshi huko Gaza ili kupata mafanikio yatakayoweza kuufariji na kuhafifisha pigo la kiintelijensia na kiusalama ulilopata kutokana na operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ya tarehe 7 Oktoba.
David Hearst, mwandishi na mchambuzi mashuhuri wa Uingereza na mhariri mkuu wa tovuti ya Middle East Eye, ambaye ameandika makala nyingi kuhusu viashiria vya kushindwa utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza tangu ilipoanza operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, ameandika yafuatayo katika makala yake mpya: "vita dhidi ya Gaza ni matokeo ya tathmini ya makosa matupu iliyofanya Israel, ambayo yameisababishia maafa ya kimaadili na kijeshi na kuchochea hasira za kimataifa dhidi ya Israel duniani kote".
Hearst amebainisha kuwa, hali halisi ya kisiasa baada ya Oktoba 7 imekuwa kinyume na matakwa ya Marekani na waungaji mkono wengine wa Israel na akasisitiza kwamba, Netanyahu na baraza lake la mawaziri la vita wamedhamiria kuiangamiza Hamas, lakini vita vya Gaza vinaweza vikawa na matokeo ya kuangamia Israel.
David Hearst
Kwa upande mwingine, muungano ambao Marekani ilitaka kuunda ili kuiunga mkono na kuisaidia Israel kukabiliana na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Yemen umesambaratika mara tu baada ya kuanzishwa.
Licha ya juhudi za Marekani za kutaka kuziingiza nchi mbalimbali katika muungano huo ili kukabiliana na mashambulizi ya Yemen dhidi ya Israel, washirika watatu wa Washington barani Ulaya wametoa jibu la kukataa kujiunga na muungano huo.
Wakati siku chache zilizopita Washington ilitangaza kuunda muungano wa jeshi la majini kwa kushirikisha nchi 10 zikiwemo Uingereza, Bahrain, Canada, Ufaransa, Italia, Uholanzi, Norway, Ushelisheli na Uhispania ili kukabiliana na kile ulichokiita vitisho vya jeshi la Yemen katika Bahari Nyekundu, duru za habari zinaripoti kusambaratika hatua kwa hatua muungano huo wa kijeshi baada ya kujiondoa washirika wa Marekani, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, Italia na Uhispania.
Tovuti ya Marekani ya "The War Zone", ambayo inajishughulisha na masuala ya kijeshi, imeandika katika ripoti kwamba: Operesheni ya Walinzi wa Fanaka(The Guardians of Prosperity) inayoongozwa na Marekani katika Bahari Nyekundu inakabiliwa na mipasuko kadhaa na mikubwa.
Ukweli ni kwamba, hatua za kijeshi ilizochukua Harakati ya Ansarullah ya Yemen dhidi ya utawala wa Kizayuni ya kuzishambulia meli za kibiashara za utawala huo katika Bahari Nyekundu ambazo ni moja ya mihimili yake mikuu ya kiuchumi, sio tu imeukanganya utawala huo ghasibu na waungaji mkono wake wakuu wasijue la kufanya, lakini kwa upande wa kiuchumi pia imeuweka kwenye mashinikizo ya kiuchumi utawala wa Kizayuni na hata nchi za Magharibi pia ya kuzitaka zikomeshe jinai zao dhidi ya watu wa Gaza.../