Ujumbe wa kuendelea maandamano ya wananchi wa Uturuki dhidi ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106444-ujumbe_wa_kuendelea_maandamano_ya_wananchi_wa_uturuki_dhidi_ya_israel
Licha za siasa za kundumakuwili za serikali ya Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki kuhusu masuala ya Palestina, wananchi wa nchi hiyo bado wanaendelea na maandamano yao ya kihamasa dhidi ya Israeli.
(last modified 2023-12-26T04:02:53+00:00 )
Dec 26, 2023 04:02 UTC
  • Ujumbe wa kuendelea maandamano ya wananchi wa Uturuki dhidi ya Israel

Licha za siasa za kundumakuwili za serikali ya Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki kuhusu masuala ya Palestina, wananchi wa nchi hiyo bado wanaendelea na maandamano yao ya kihamasa dhidi ya Israeli.

Kuhusiana na jambo hilo, wananchi wa Uturuki walifanya maandamano makubwa karibuni mjini Ankara ikiwa ni katika kulaani mauaji ya kimbari huko Palestina, mashambulizi ya mara kwa mara ya utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya raia wa Gaza na pia kuunga mkono taifa la Palestina. Maandamano hayo, ambayo yaliandaliwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali huko Ankara, yalianzia katika kituo cha metro cha Atatürk na kumalizikia kwa taarifa ya pamoja ya kutetea Gaza katika uwanja wa Anadolu.

Washiriki wa Maandamano Makubwa ya Gaza katika mji mkuu wa Uturuki, kwanza walitoa heshima zao kwa waandishi wa habari ambao waliuawa shahidi katika mashambulizi ya utawala wa kibaguzi wa Israel huko Gaza. Tokea tarehe 7 Novemba hadi sasa zaidi ya Wapalestina elfu 20 na 500 wameuawa shahidi katika Ukanda wa Gaza. Takwimu za mauaji ya kimbari na ya kizazi dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina zinaonyesha kiwango cha jinai zinazotekelezwa na utawala katili wa Kizayuni huko Gaza. Katika hali hiyo ni wazi kuwa, nchi nyingine duniani ikiwemo Marekani na waitifaki wake bado zinaendeleza uungaji mkono wao kwa jinai hizo za Israel huko Gaza.

Maandamano ya wananchi wa Uturuki

Msimamo wa sasa wa serikali za Magharibi kuhusiana na matukio ya Gaza si tu kwamba hauendani na siasa zao za kuunga mkono haki za binadamu, bali pia unahimiza kuendelea jinai na uhalifu wa utawala huo ghasibu katika eneo la Gaza. Kuhusiana na jambo hilo, misimamo ya wanasiasa wa Uturuki haiende sambamba na ya wananchi wa nchi hiyo. Hata wachambuzi wa Kituruki pia wamechukua misimamo mizuri na iliyo dhidi ya jinai za Israel huko Gaza.

Licha ya wachambuzi wa kisiasa wa Uturuki kukosoa jinai za utawala wa Kizayuni, serikali ya Recep Tayyip Erdoğan inafuatilia masuala kama vile mazungumzo na jitihada za kutangaza usitishwaji vita kati ya Palestina na Israel. Serikali ya Erdogan hata imejipusha kumfukuza balozi wa Israel mjini Ankara. Kuhusiana na hilo, Ahmad Tashgatiren, mmoja wa wachambuzi mashuhuri wa Uturuki kuhusu masuala ya kisiasa na usalama, hivi karibuni aliandika katika uchambuzi wake kuhusu mtazamo wa Magharibi kuhusu matukio ya Gaza kama ifuatavyo:

Mashambulizi ya kinyama dhidi ya Gaza bado yanaendelea. Idadi ya wakimbizi inazidi kuongezeka kila siku. Kunashuhudiwa kila siku kuendelea kuuawa raia wasio na hatia hasa watoto na wanawake. Pamoja na hayo, serikali za Magharibi zimeendelea kuunga mkono jinai za Israel huko Gaza.

Mchambuzi huyo maarufu wa Kituruki pia amepinga uhusiano wa Ankara na Washington na kuandika:

'Uturuki inatoa kipaumbele kwa uhusiano wake na nchi za Magharibi. Uturuki ni nchi ya pili yenye nguvu ya kijeshi katika Muungano wa Ulinzi wa Magharibi. Inashangaza kwamba Joe Biden hakutani na Recep Tayyip Erdogan! Rais huyo wa Marekani ametoka maelfu ya kilomita na kumkumbatia Waziri Mkuu wa Israel, lakini hayuko tayari kukutana na Rais wa Uturuki.'

Ungaji mkono wa raia wa Uturuki kwa wakazi wa Gaza

Ukweli huu unaonyesha kuwa hata katika hali ya mgogoro, Marekani imeitenga serikali ya Uturuki kati ya washirika wake, na hivyo kushindwa katika mtihani wa Gaza. Katika hali hiyo ya kuchanganyikiwa serikali za Magharibi, walimwengu na hata raia wa nchi za Magharibi zenyewe, wamejitokeza kwa wingi na kushinda mtihani huo mkubwa wa Mwenyezi Mungu. Radiamali mbalimbali, kujiuzulu na upinzani bado unaendelea katika nchi za Magharibi, na maandamano ya kufungamana na wananchi  wa Gaza huko New York na Washington yana umuhimu mkubwa na yanaonesha kuwa, wananchi wa Magharibi, tofauti na serikali zao, hawako tayari kuhusishwa na jinai za Israel huko Gaza.

Makumi ya wasanii wa filamu nchini Marekani (Hollywood) katika barua ya pamoja kwa Rais Joe Biden, wamemtaka aulazimishe utawala wa Israel ufikie makubaliano ya kusitisha mapigano na harakati ya Hamas. Mashirika ya wanaharakati wa haki za binadamu wa Marekani pia yamemtaja Benjamin Netanyahu kuwa mhusika na mtenda jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza na wamejitahidi kumshtaki katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Kwa upande mwingine, serikali za Ulaya zinaunga mkono kikamilifu  jinai na mauaji ya halaiki ya Israel katika Ukanda wa Gaza. Hatua ya serikali ya Ujerumani kuhusiana na Bi Adnia Shebli, mwandishi wa Palestina, na za serikali ya Uswizi za kufuta tamasha la mcheza muziki maarufu wa Kituruki Fazel Sai kwa sababu ya kukosoa jinai za Israeli na kutonyamaza kuhusu mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala huo huko Gaza ni mfano mdogo tu wa sera za serikali za Magharibi kuhusu jinai za Israel dhidi ya wakazi wa Gaza.

Wakati huo huo, uungaji mkono wa mara kwa mara wa Waturuki kwa wananchi wa Gaza pia umefichua ukweli wa kugongana misimamo ya serikali ya Uturuki na wananchi wa nchi hiyo, ambapo wananchi waliomchagua karibuni Recep Tayyip Erdogan katika uchaguzi wa rais wana misimamo inayokinzana na serikali kuu ya Ankara na bila shaka maamuzi yao yana umuhimu mkubwa kuliko siasa za viongozi wanaotawala nchini humo. Kwa kutilia maanani jinai zinazoendelea kila siku za Israel katika Ukanda wa Gaza, hapana shaka kuwa maandamano ya mataifa ya Kiislamu wakiwemo wananchi Waislamu wa Uturuki dhidi ya jinai za Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yataendelea kushuhudiwa katika siku zijazo.