Maandamano dhidi ya Benjamin Netanyahu ndani ya Israel na kimataifa
Huku utawala haramu wa Israel ukiendeleza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza maandamano dhidi ya Waziri Mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu yameenea ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).
Maelfu ya watu waliandamana kumpinga Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Januari 6, 2024 mjini Tel Aviv ambapo polisi wa utawala huo waliwashambulia waandamanaji.
Sababu kuu ya maandamano hayo ni kushindwa utawala wa Kizayuni kuwakomboa mateka wa Kizayuni huko Gaza. Mbali na familia za mateka, maelfu ya watu wengine pia walishiriki katika maandamano hayo.
Jambo muhimu katika madai ya waandamanaji ni matakwa yao ya kumtaka Netanyahu ajiuzulu na kufanyika uchaguzi wa mapema wa bunge.
Kwa upande mmoja, familia za mateka wa Kizayuni zimekuwa changamoto kubwa kwa Netanyahu na baraza lake la mawaziri, na kwa upande mwingine, waandamanaji wanaamini kuwa vita vya Gaza mbavyo vimekuwa vikiendelea kwa miezi mitatu sasa vimeathiri na kuvuruga maisha yao.
Wafanyakazi wengi wamelazimishwa kujiunga na jeshi na kuelekea vitani Ghaza, biashara nyingi zimefungwa na watu kunyimwa vyanzo vyao vya mapato. Kwa hiyo, huku wakitaka vita vikomeshwe, waandamanaji pia wanasisitiza kujiuzulu kwa Netanyahu na kufanyika uchaguzi mkuu wa mapema. Wakati huo huo, moja ya sababu za Netanyahu kuendeleza vita ni uhakika kuwa punde vita vitakapomalizika atondolewa madarakani.
Nukta muhimu ni kwamba, waandamanaji hasa wa familia za Wazayuni wanaoshikiliwa mateka Gaza wanasisitiza kuachiliwa huru mateka hao katika hali ambayo mazungumzo ya usitishaji vita kati ya utawala wa Kizayuni na Hamas pia yalisitishwa baada ya utawala huo kumuua kigaidi Saleh al-Arouri naibu mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas ambaye alikuwa anaishi Beirut, Lebanon.
Kwa hakika, kusimamishwa mazungumzo ya kusitisha mapigano ni sababu nyingine ya kushadidi maandamano dhidi ya Netanyahu katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
Wakati maandamano hayo dhidi ya Netanyahu yakifanyika katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, wananchi wa Uingereza nao wametangaza uungaji mkono wao kwa Palestina kwa kufanya maandamano huko London, mji mkuu wa nchi hiyo na kutaka balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel afukuzwe nchini humo.
Maelfu ya wananchi wa Uingereza wametia saini ombi la kutaka afukuzwe Tzipi Hotovli, balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mjini London. Sababu ya ombi hilo la waandamanaji wa Uingereza ni uungaji mkono wa Tzipi Hotovli kwa mauaji ya kimbari huko Gaza.
Maandamano ya wananchi wa Uingereza ambayo bila shaka yanafanyika sambamba na maandamano ya wananchi wa nchi mbalimbali kote duniani yanaonesha kuwa kwa upande mmoja maoni ya wananchi katika nchi zinazouunga mkono utawala wa Kizayuni yanakinzana na siasa za serikali. Ni wazi kuwa wananchi waliowengi duniani kote wanaunga mkono Palestina, na kwa upande mwingine, utawala wa Kizayuni pia umeshindwa katika vita kijeshi na pia katika fikra za umma..
Kwa msaada wa vyombo vya habari vya Marekani na Ulaya, utawala wa Kizayuni unajaribu kuhadaa walimwengu kuwa eti vita dhidi ya Gaza ni kielelezo cha kujitetea halali, lakini simulizi hii ya Wazayuni inapingwa waziwazi na maoni ya walimwengu ambao wanaamini kuwa vita hivyo ni mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita.
Kwa kuzingatia hayo, tunaweza kusemwa kuwa utawala wa Kizayuni unakabiliwa na mashinikizo ya maoni ya umma ndani ya Israel na katika uga wa kimataifa. Hivyo kuendelea vita dhidi ya Gaza kutapelekea utawala wa Kizayuni wa Israel upate hasara katika pande zote.
Kama ilivyotajwa na shakhsia wengi wa Kizayuni, kuendelea vita dhidi ya Gaza ni kwa maslahi ya binafsi ya Benjamin Netanyahu.