Kushtadi mipasuko ya ndani katika utawala wa Kizayuni wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107262-kushtadi_mipasuko_ya_ndani_katika_utawala_wa_kizayuni_wa_israel
Katika hali ambayo, zimepita siku 100 tangu kuanza vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza, vita hivyo vinaonekana kushadidisha migawanyiko na mipasuko ya ndani katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).
(last modified 2024-01-16T03:02:53+00:00 )
Jan 16, 2024 03:02 UTC
  • Kushtadi mipasuko ya ndani katika utawala wa Kizayuni wa Israel

Katika hali ambayo, zimepita siku 100 tangu kuanza vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza, vita hivyo vinaonekana kushadidisha migawanyiko na mipasuko ya ndani katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Kabla ya kuanza vita vya Gaza, maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yalikuwa yakishuhudia mgawanyiko wa wazi wa kisiasa na kijamii. Mpasuko huo, ulidhihirika katika fremu ya kufanyika maandamano mtawalia ya mamia ya maelfu ya watu dhidi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu na baraza lake la mawaziri. Hata kabla ya baraza la mawaziri la Netanyahu kushika hatamu za uongozii huko Israel, mgawanyiko wa kijamii na kisiasa ndani ya Israel ulikuwa ukionekana wazi na bayana kabisa ambapo, vyama vya siasa na viongozi wao hawakuweza kufikia mwafaka wa kuunda baraza la mawaziri na kuuondoa utawala huo katika mkwamo wa kisiasa.

Ni kwa sababu hiyo, ndio maana kulifanyikka chaguzi 5 za bunge katika kipindi cha miaka 4, na matokeo ya uchaguzi wa tano, ambao ulifanyika mwishoni mwa 2022, yakawa ni kuingia madarakana baraza la mawaziri la muungano la Netanyahu likiundwa na wanasiasa wabaguzi na wenye misimamo ya kufurutu ada. Kuingiia madarakani baraza hilo kulishadidisha mgawanyiko uliokuweko hapo kabla.

Vita vya Gaza, ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa zaidi ya siku 100 sasa, navyo vimezidisha mpasuko huo. Suala hili limedhihirika kwa namna tofauti. Kuna hitilafu kubwa kati ya Netanyahu na baadhi ya mawaziri wake, hasa Waziri wa Vita. Waziri wa Vita Yoav Gallant amemshutumu Netanyahu kwamba, anakwamisha utendajikazi wa wizara hiyo, na wakati huo huo hali ya kutoaminiana pia inaonekana kutanda kati ya pande hizo.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

 

Kanali ya 12 ya Televisheni ya utawala ghasibu wa Israel imetangaza kuwa, ofisi ya Netanyahu inaamini kwamba, ofisi ya Gallant ilifichua mambo yaliyozungumzwa kwenye mkutano wake wa faragha na Netanyahu. Hapo awali, Gallant alisema kuwa, Netanyahu hampatii taarifa za siri kuhusiana na vita vya Gaza, wakati yeye ni waziri wa vita wa utawala huo.

Tofauti zilizopo ndani ya baraza la mawaziri la Israel hazishii tu kwenye tofauti kati ya waziri mkuu na waziri wa vita, bali pia kuna hali ya kutoaminiana na mvutano kati ya mawaziri wengine wa baraza la Netanyahu linalolegalega. Itamar Ben-Gvir ni mmoja wa mawaziri walioacha kanuni zote za mchezo wa kisiasa na kuweka misimamo mikali kuwa ndio ajenda, suala ambalo lilikabiliwa na pingamizi la Yoav Gallant, Waziri wa Vita na baadhi ya wajumbe wengine wa baraza la mawaziri na hata kusababisha kuzuka mvutano wa maneno kati ya wajumbe na hiivyo kupelekea kutofanyika vikao vya Baraza la Mawaziri.

Sambamba na tofauti hizi, pia kuna mgawanyiko ndani ya baraza la mawaziri la vita. Benny Gantz ambaye ni mkosoaji wa Netanyahu na si mjumbe wa baraza la mawaziri bali ni mjumbe wa baraza la vita la utawala wa Kizayuni alichapisha picha yake inayomuonyesha akishiriki katika maandamano ya familia za mateka wa Kizayuni mjini Tel Aviv. Waandamanaji walioshiriki maandamano hayo, ambao idadi yao ilifikia maelfu kadhaa, walitoa nara dhidi ya Netanyahu na kutaka baraza lake la mawaziri livunjwe na kuitishwa uchaguzi wa mapema.

Mamia ya wanajeshi wa utawal haramu wa Israel wameuawa tangu kuanza kwa vita vya Gaza

 

Kwa maneno mengine ni kuwa, kwa upande mmoja, Gantz ni mjumbe wa baraza la mawaziri la vita la utawala wa Kizayuni, na kwa upande mwingine, kama walivyo wakosoaji wengine wa Netanyahu, kama vile Yair Lapid, bado anajaribu kumuondoa Netanyahu madarakani.

Kushindwa kwa Netanyahu kufikia malengo yake ya kijeshi katika vita vya Gaza kumezidisha migawanyiko hii ya kisiasa. Wakosoaji, hata ndani ya baraza la mawaziri na ndani ya chama cha Likud, wanaamini kuwa Netanyahu anajaribu kusalia madarakani kwa kurefusha vita vya Gaza, huku akiisababishia Israel gharama kubwa wakati wa vita, ikiwa ni pamoja na kuuawa mamia ya wanajeshi wa Israel na zaidi ya 4000 kujeruhiwa.