Kupungua pakubwa uungaji mkono kwa utawala wa Kizayuni duniani
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Morning Consult yanaonyesha kuwa uungaji mkono wa kimataifa kwa utawala wa Kizayuni umepungua sana kufuatia vita vilivyoanzishwa na utawala huo haramu dhidi ya wakazi wa Palestina wa Ukanda wa Gaza.
Taasisi ya Morning Consult imefanya uchunguzi wake huo wa maoni katika nchi 43 kwenye muda wa mwezi mmoja; na katika kila nchi watu 300 hadi 600 wameshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni.
Uungaji mkono wa wazi kwa utawala huo duniani ambao unapatikana baada ya kuondoa asilimia ya wale wanaoupinga na wenye fikra hasi kuhusu utawala wa Kizayuni mkabala wa wale wenye mitazamo chanya umepungua kwa asilimia 18.5 tangu mwezi Septemba hadi Disemba mwaka jana. Takwimu zinaonyesha kuwa, uungaji mkono wa fikra za walimwengu kwa utawala wa Kizayuni umepungua katika nchi 42 kati ya nchi 43 duniani ambako uchunguzi huu wa maoni umefanyika.
Kupungua pakubwa uungaji mkono wa watu katika nchi mbalimbali duniani kwa utawala wa Kizayuni kunabainika wazi na kupata maana kwa kuzingatia jinai kubwa za ukatili na maangamizi ya kizazi yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na utawala huo ghasibu huko Ukanda wa Gaza katika vita vyake unavyoendeleza dhidi ya makundi ya mapambano ya Palestina khususan harakati ya muqawama ya Hamas. Utawala wa Kizayuni kwa miongo kadhaa sasa pamoja na kutumia suala la Holocaust kama kisingizo na kujionesha kuwa ni mdhulumiwa kimataifa kwa upande mmoja; na kwa upande wa pili kufanya juhudi za kuyaonesha mapambano ya wananchi wa Palestina kuwa ni ugaidi, umeshindwa hata hivyo kuidhihirishia dunia taswira yake chanya.
Pamoja na hayo, taswira hii imeonekana kwa uwazi zaidi katika muongo mmoja uliopita kupitia vita vya pande kadhaa vya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Gaza, na pia vitendo haramu na viliyo kinyume cha sheria kama ujenzi wa vitongoji vingi vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na huko Quds inayokaliwa kwa mabavu huku Israel ikiendeleza njama zake za kuwafukuza Wapalestina kwenye makazi na adhi zao na kujenga ukuta wa kibaguzi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kinachoumiza zaidi kuhusu vita vya kikatili na vya kijinai vinavyoendeshwa na utawala wa Kizayuhu huko Gaza hivi sasa ni kuona haki za binadamu zinapuuzwa. Idadi ya raia waliouliwa shahidi huko Gaza ambayo imepindukia watu elfu 25 sambamba na kubomolewa nyumba na miundombinu na pia kusababisha asilimia 90 ya wakazi wa eneo hilo kuwa wakimbizi yote haya yanaonyesha ukatili na ukandamizaji mkubwa unaofanywa na Wazayuni.
Ni wazi kuwa vita vya Gaza na sisitizo la utawala wa Kizayuni la kuendeleza mashambulizi yake ya jinai katika eneo hilo kwa kisingizio cha kujilinda, jambo ambalo bila ya shaka linaambatana na uungaji mkono kamili na wa pande zote wa Marekani ikiwa ni mshirika wa kiistratijia wa Israel na baadhi ya nchi za Ulaya kama Ujerumani na Uingereza vimeathiri vibaya mno taswira ya Israel duniani kote.
Wananchi huko China, Afrika Kusini, Brazil na katika nchi nyingine za Amerika ya Latini ambao huko nyuma walikuwa na mtizamo chanya kuhusu utawala wa Kizayuni, hivi sasa wana mtizamo mbaya na hasi kuhusu utawala huo ghasibu. Wananchi wa nchi kama Japan, Korea ya Kusini na Uingereza pia ambao kitambo nyuma walikuwa na mtizamo chanya kuhusu Israel hivi sasa wanashuhudia kuongezeka mitizamo hasi na mibaya kuhusu utawala wa Kizayuni. Uungaji mkono wa wazi kwa utawala wa Kizayuni huko Japan umepungua kutoka chini ya sifuri 62 hadi chini ya sifuri 29.9, huko Korea Kusini umezidi kuporomoka kutoka chini ya sifuri 5.5 hadi chini ya sifuri 47.8 na nchini Uingereza umetoka chini ya sifuri 17.1 hadi chini ya sifuri 29.8. Sant Frisby, Naibu Mkurugenzi wa idara ya taarifa za kisiasa katika taasisi ya Morning Consult, anasema: Data hizi zinaonyesha njia ngumu ambayo Israeli inaipitia hivi sasa katika jamii ya kimataifa.
Jambo la kufurahisha ni kwamba hata huko Marekani kwenyewe; nchi ambayo ni mshirika wa kistratijia wa Israel na ndiyo nchi pekee tajiri ambako utawala wa Kizayuni bado una uungaji mkono wa wazi; kiwango cha uungaji mkono na kukubalika utawala huo kimekuwa kikipungua; ambapo tangu mwezi Septemba hadi Disemba mwaka jana kiwango hicho kilipungua kutoka asilimia18.2 hadi asilimia 16. Wakati huo huo uchunguzi huu wa maoni umeonyesha pia kuwa, kuendelea uungaji mkono wa pande zote ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni kumeisababishia matatizo na ukosoaji mkubwa Washington kimataifa na khususan katika Ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.
Hii ni katika hali ambayo, kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza ambazo hadi sasa zimepelekea kuuliwa shahidi Wapalestina zaidi ya elfu 25 na kujeruhiwa wengine zaidi ya elfu 62 kumeshadisha ghadhabu na ukosoaji wa kimataifa dhidi ya jinai za Israel; kiasi kwamba maandamano makubwa yamekuwa yakifanyika kila siku katika pembe mbalimbali duniani khususan katika nchi za Ulaya na Marekani. Wafanya maandamano wamekuwa wakipiga nara wakitaka kukomesha haraka iwezekanavyo vita huko Gaza na kufikishiwa misaada ya kibinadamu raia wa Kipalestina wa ukanda huo.
Katika upande mwingine, hii ni mara ya kwanza katika ngazi ya nchi duniani ambapo Israel imefunguliwa kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kutokana na jinai inazowafanyia Wapalestina huko Gaza. Kuhusiana na hilo, Mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini The Hague, wiki iliyopita ilikubali kusikiliza malalamiko ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni na kutangaza kuwa, inachunguza tuhuma za mauaji ya halaiki zinazofanywa na utawala huo huko Gaza.
Masuala yote haya yanaonyesha mwelekeo wa wazi wa kuporomoka taswira ya utawala wa Kizayuni duniani; jambo ambalo kwa hakika limekuwa na taathira hasi kwa nguvu laini ya utawala huo, na wakati huo huo yanazidisha mashinikizo ya fikra za waliowengi kwa nchi zinazoihami Israel hasa Marekani ili iulazimishe utawala huo haramu usimamishe vita huko Gaza.