Wayemeni waunga mkono mashambulizi dhidi ya meli zinazoelekea Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107722-wayemeni_waunga_mkono_mashambulizi_dhidi_ya_meli_zinazoelekea_israel
Kwa mara nyingine tena mamilioni ya wananchi wa Yemen wamefanya maandamano makubwa na kutangaza uungaji mkono wao kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Ukanda wa Gaza na vilevile hatua za kijeshi dhidi ya meli inazoelekea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
(last modified 2024-01-28T04:14:24+00:00 )
Jan 28, 2024 04:14 UTC
  • Wayemeni waunga mkono mashambulizi dhidi ya meli zinazoelekea Israel

Kwa mara nyingine tena mamilioni ya wananchi wa Yemen wamefanya maandamano makubwa na kutangaza uungaji mkono wao kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Ukanda wa Gaza na vilevile hatua za kijeshi dhidi ya meli inazoelekea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.

Hatua ya  Wayemeni ilikuwa na jumbe muhimu ambazo pia zilitangazwa katika nara na kauli mbiu za waandamanaji.

Ujumbe wa kwanza ni kuwa, watu wa Yemen wanafahamu vyema na kuhisi hali ya sasa ya watu wa Gaza kwa sababu walishuhudia pia vita visivyo na usawa na vya kidhuluma kwa muda wa miaka 8 na kukabiliwa na maafa makubwa ya binadamu kutokana na vita hivyo. Hivyo watu wa Yemen wanaelewa vyema zaidi machungu na mateso yanayowapata wananchi wa Ukanda Gaza. Ni kutokana na ukweli huo ndiyo maana Wayemeni wamekariri katika maandamano yao kwamba: ''Yemen na Palestina ziko katika handaki moja ya mapambano.''

Ujumbe wa pili ni kwamba, hatua ya jeshi la Yemen dhidi ya meli zinazoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina (Israel) imechukuliwa kwa himaya ya wananchi, na Wayemeni wanaunga mkono hatua hiyo kwa ajili ya kuhitimisha vita na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Gaza. Tangu siku za nyuma, na kwa lengo la kuliunga mkono taifa la Palestina, wanajeshi wa Yemen wamekuwa wakizuia meli za Israel zinazoelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu kupita katika Bahari Nyekundu, na mara kwa mara wamekuwa wakizilenga  kwa makombora na ndege zisizo na rubani.

Kuwa tayari wayemen kukabiliana na madai

Ujumbe wa tatu ni kwamba, wananchi wa Yemen wanaamini kuwa, utawala wa Kizayuni unaendeleza vita na jinai dhidi ya watu wa Gaza kwa uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya ikiwemo Uingereza. Hatua za hivi karibuni za Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen kwa madai ya kulinda usafiri huru wa meli kwa hakika ni kuendelea kuunga mkono mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza. Na ni kwa sababu hiyo, ndipo kauli mbiu ya maandamano ya wananchi wa Yemeni ikazilenga Marekani na Uingereza.

Ujumbe wa nne ni kwamba mashambulizi ya Marekani na waitifaki wake dhidi ya Yemen hayatazuia mashambulizi wanamapambano shupavu wa nchi hiyo dhidi ya meli zinazopeleka bidhaa huko Israel, kwa sababu hatua ya jeshi la serikali ya Sana'a inaungwa mkono kwa dhati na wananchi. Hapa tunaweza kusema kuwa, kama mojawapo ya sababu za mashambulizi ya Marekani na waitifaki wake dhidi ya Yemen ni kuzishinikiza fikra za wananchi dhidi ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa, basi maandamano ya mamilioni ya Wayemeni Ijumaa iliyopita yamebatilisha mipango ya mabeberu hao.

Meli ya Israel iliyotekwa katika Bahari Nyekundu

Shirika rasmi la habari la Yemen limeripoti kuhusiana na suala hilo kuwa, wakazi wa Sana'a pamoja na kutoa nara dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel wametangaza utayarifu wao wa kukabiliana na Washington, London na Tel Aviv na kusisitiza kuwa wataendeleza mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni hadi pale Quds tukufu na ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zitakapokombolewa. Wananchi wa Sana'a pia wamesisitiza katika taarifa yao kuwa "Marekani ndio mama wa ugaidi", na kwamba mashambulizi ya Marekani na Uingereza hayatazuia mapambano ya taifa la Yemen kwa sababu kulisaidia taifa la Palestina ni jukumu lao la kidini, kimaadili na kibinadamu.