Yemen: Siku ya Kimataifa ya Quds imeibakisha hai kadhia ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i110258-yemen_siku_ya_kimataifa_ya_quds_imeibakisha_hai_kadhia_ya_palestina
Katibu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema kuwa, Siku ya Kimataifa ya Quds imeyabakisha hai mapambano ya ukombozi wa Palestina.
(last modified 2024-04-04T08:01:51+00:00 )
Apr 04, 2024 08:01 UTC
  • Yemen: Siku ya Kimataifa ya Quds imeibakisha hai kadhia ya Palestina

Katibu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema kuwa, Siku ya Kimataifa ya Quds imeyabakisha hai mapambano ya ukombozi wa Palestina.

Kesho ni Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mwaka huu. Ijumaa ya kesho inasadifiana na Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo huwa inaadhimishwa katika siku kama hiyo kila mwaka kwa ubunifu wa Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Yasir al-Houri, Katibu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema hayo leo Alkhamisi katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la IRNA na kuongeza kuwa, kutangazwa Siku ya Kimataifa ya Quds kumewakasirisha Wazayuni wakiwemo pia Wazayuni wa Marekani na Uingereza kwani moyo ya muqawama, mapambano na matumaini ya kukombolewa Palestina na maeneo matakatifu ya umma wa Kiislamu umehuishwa kwa kutangazwa siku hiyo muhimu katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Yasir al-Houri, Katibu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen

 

Ameongeza kuwa, mwaka huu Siku ya Kimataifa ya Quds inabidi iadhimishwe kwa kulaani vitendo vya wale viongozi wa madola ya Waislamu waliotangaza uhusiano wa kwaida na utawala wa Kizayuni na iwe ni fursa pia ya kuleta umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.

Katibu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen aidha amesema, ujumbe muhimu zaidi wa Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu kwa mataifa ya dunia yaliyonyamazia kimya jinai za kutisha za Wazayuni ni kuyataka mataifa hayo na waungaji mkono wa Israel waone aibu na wawe huru katika nafsi zao.

Pia amesema, Siku ya Kimataifa ya Quds ni ushindi mkubwa wa kadhia nzima ya Palestina.