Watu 200 wafariki dunia kwa janga la mafuriko nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i111644-watu_200_wafariki_dunia_kwa_janga_la_mafuriko_nchini_afghanistan
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kwa akali watu 200 wamefariki duniani kwa mafuriko kaskazini mwa Afghanistan.
(last modified 2024-05-11T08:04:07+00:00 )
May 11, 2024 08:04 UTC
  • Watu 200 wafariki dunia kwa janga la mafuriko nchini Afghanistan

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kwa akali watu 200 wamefariki duniani kwa mafuriko kaskazini mwa Afghanistan.

Maelfu ya nyumba ziliharibiwa wakati wa mafuriko hayo katika jimbo la Baghlan baada ya mvua kubwa ya jana Ijumaa kusababisha mafuriko makubwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji IOM limetangaza kuwa, makazi 1,500 ya watu katika wilaya ya Baghlani Jadid yameharibiwa ambapo pia zaidi ya watu 100 walithibitishwa kufariki dunia.

Takwimu hizo pia zimethibitishwa na idara ya kukabiliana na majanga ya kitaifa nchini Afghanistan.

Maafisa wa serikali ya Taliban kwa upande wao wamesema kwamba watu 62 walifariki usiku wa Ijumaa pekee.

Msemaji wa utawala wa Taliban Zabihullah Mujahid amethibitisha kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba wamewapoteza watu katika mafuriko hayo bila ya kubainisha waliofariki na waliojeruhiwa.

 

Licha ya kutoweka wazi idadi ya wahanga wa mafuriko hayo, lakini amewaambia waandishi wa habari kuwa kuna watu wengi ambao wamefariki dunia kufuatia janga hilo la mafuriko.

Kwa upande wake Abdul Mateen Qani, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya serikali ya Taliban ameziambia duru za habari kwamba, watu 133 wamethibitishwa kufariki duniani kwa maafa ya mafuriko nchini Afghanistan.

Picha zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mafuriko ya maji yakipita kwenye nyumba katika vijiji kadhaa, na kufanya uharibifu mkubwa.