Israel yashadidisha ukatili, Wapalestina 450,000 waikimbia Rafah
Umoja wa Mataifa umesema eneo kubwa la mji wa Gaza sasa limekuwa “Mji uliotelekezwa.” Hayo yaliripotiwa na mashirika ya umoja huo yanayoshughulikia masuala ya misaada ya kibinadamu siku ya Jumanne na kuongeza kuwa Wapalestina wapatao 450,000 wamelazimika kuondoka eneo la Rafah kutokana na kushadidi mashambulizi ya Israel.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) katika ujumbe wake kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X kutokea eneo la Magharibi mwa Rafah limeandika: "Mitaa haina watu Rafah wakati familia zikiendelea kukimbia kutafuta eneo salama …. UNRWA inakadiria takriban watu 450,000 wamelazimishwa kuyakimbia makazi yao tangu tarehe 6 Mei."
Haya yanajiri huku utawala haramu wa Israel ukiendeleza mashambulizi ya anga dhidi ya Rafah licha ya mashirika ya umoja wa mataifa kuonya kuhusu madhara ya mashambulizi hayo.
Wengi wa wale waliolazimishwa kuondoka mashariki mwa Rafah tayari walikuwa wameyahama makazi yao kwingineko Gaza katika kipindi cha miezi saba iliyopita, ofisi ya Umoja wa Mataifa imeeleza.
Likipazia sauti hofu ya watu wa Gaza, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO limeripoti kuwa uvamizi wa Israel huko Rafah umehatarisha upatikanaji wa huduma za afya, utoaji wa huduma za afya na utoaji wa vifaa vya kuokoa maisha.
WHO imebainisha kuwa wadau wake wanaoshughulikia misaada ya matibabu huko Gaza "wanahitaji kiwango cha chini cha lita 46,000 za mafuta kila siku kwa ajili ya shughuli zao."
Hayo yanaripotiwa wakati ambao Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto ,UNICEF, limetangaza kuwa watoto karibu 15,000 wa Kipalestina ni miongoni mwa watu zaidi ya 35,000 waliouawa hadi sasa katika mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza huko Palestina tokea Oktoba 7, 2023.