Msemaji wa UNRWA atahadharisha kuhusu hali ya mji wa Rafah
Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA) ameitaja hali ya mji wa Rafah huko kusini mwa Ukanda wa Gaza kuwa sawa na mji uliotelekezwa uliosalia magofu.
Louise Wateridge Msemaji wa shirika la UNRWA ambaye yupo katika mji wa Rafah amesema katika ujumbe aliotuma katika mtandao wa X yaani Twitter ya zamani kuwa: Familia zilizopo kusini mwa mji wa Rafah huenda zikaelekea upande wa magharibi wa mji huo.
Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina amesema hivi akibainisha wazi kuhusu hali ya mji wa Rafah: Sehemu kubwa ya mji huo hivi sasa imekuwa magofu.
Wateridge amesema kuwa ni vigumu kuamini kuwa zaidi ya watu milioni moja hadi kufikia wiki hii walikimbilia mji huo kwa ajili ya hifadhi.
Kuhusiana na suala hili, Stephane Dujjaric Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa jana Jumanne alisema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa Katibu Mkuu Antonio Guterres amesikitishwa na kuongezeka harakati za kijeshi katika mji wa Rafah na maeneo ya kandokando, zinazotekelezwa na wanajeshi wa Israel.
Baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni tarehe 6 mwezi huu lilipasisha kuanza mashambulizi dhidi ya mji wa Rafah ambapo jeshi la utawala huo bandia limeanza mashambulizi dhidi ya mji huo tangu Jumanne iliyopita licha ya upinzani wa kimataifa.
Kwa utaratibu huo, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni upande wa kivuko cha Rafah yamefunga njia pekee ya mawasiliano ya raia wa Palestina wa Ukanda wa Gaza na ulimwengu wa nje.