Wazayuni washambulia misafara ya misaada ya kibinadamu huko Gaza
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimeripoti kuwa, walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakishambulia malori yanayobeba misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Gaza karibu na mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Gazeti la Kiibrania la Ha'aretz, likinukuu vyanzo vya usalama, limeripoti kuwa kabla ya hapo, Wazayuni walirarua vifurushi vya chakula na magunia ya nafaka ya misafara ya misaada ya kibinadamu katika maeneo tofauti, iliyokuwa inaelekea Ukanda wa Gaza, na kuiacha kando kando ya barabara. Hii inaonyesha kuwa, Wazayuni wanaendelea kufanya mashambulizi mseto dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza. Mauaji, uchinjaji, ubakaji, kushadidisha njaa na kufurushwa na vikosi mbalimbali vya usalama na walowezi wa Kizayuni ni vitendo vya jinai vinavyoendelea kufanywa dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Gaza, ambapo Wazayuni wanawanyima watu madhulumu wa Gaza chakula, dawa na hata maji ya kunywa. Mohsen Rui Safat, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: 'Uhalisia wa medani ya vita vya Gaza unathibitisha kushindwa kikamilifu utawala wa Kizayuni.'
Kwa kuua shahidi zaidi ya watu 35,000 wa Gaza na kuharibu asilimia 90 ya eneo hilo, utawala huu si tu kwamba umeshindwa kufikia malengo yake, yakiwemo ya kuangamiza Hamas na kukomboa mateka, bali kila siku unaendelea kuzama kwenye kinamasi cha vita vya Gaza. Hivyo Wazayuni wameamua kuendelea kutekeleza jinai mbalimbali za kutisha dhidi ya watu wa Gaza kwa matumaini kwamba huenda wakapata ushindi na hivyo kufidia kushindwa kwao na vilevile kusimamisha mapambano ya ukombozi ya Wapalestina. Wamefunga vivuko vyote vya kuingia Gaza na wakati huo huo kuwabana Wapalestina kwa kuwanyima chakula na kuwaongezea njaa kwa matumaini kuwa wataweza kuwashinikiza wanamapambano wa Hamas na hatimaye kuwalazimisha kulegeza msimamo kwenye meza ya mazungumzo.
Hii ni pamoja na ukweli kwamba mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada ya kibinadamu ni kitendo cha kinyama kabisa kinachofanyika chini ya ushirikiano wa Marekani na kimya cha nchi za Ulaya. Ni kutokana na hilo ndipo Rais Michael Higgins wa Ireland, akalaani kupitia taarifa, shambulio hilo la walowezi wa Kizayuni dhidi ya misafara ya misaada ya kibinadamu inayokwenda Gaza. Huku akibainisha kuwa kimya kuhusu shambulio dhidi ya misafara ya misaada ya kibinadamu inayopelekwa Gaza kitakuwa na athari mbaya kwa kila mwanachama wa Umoja wa Ulaya, ameongeza kwamba kitendo hicho kinatisha.
Akizungumzia kifo cha mfanyakazi mmoja wa Umoja wa Mataifa huko Rafah na uharibifu uliofanywa dhidi ya misaada ya kibinadamu iliyotumwa kwa watu wa Palestina, Higgins amesisitiza kwamba wale wote wanaounga mkono haki za binadamu, misaada ya kibinadamu, Umoja wa Mataifa na hati yake wanapaswa kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi yanayofanywa dhidi ya misafara ya misaada muhimu ya kibinadamu inayokusudiwa kuwafikia watu wa Gaza. Amesema hilo linatokana na ukweli kuwa kimya cha wale wanaodai kutetea haki za binadamu kitashajiisha kufanyika mashambulizi zaidi ya Wazayuni dhidi ya misafara ya kibinadamu. Kuuawa karibu wafanyakazi 700 wa mashirika ya misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni kunabainisha wazi ukubwa wa maafa ya kibinadamu yanayofanywa na utawala huo katika eneo hilo.
Mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada ya kibinadamu yanafanyika huku Wapalestina huko Gaza wakikabiliwa na baa la njaa ambapo watoto wachanga wanaaga dunia wakiwa mikononi mwa mama zao kwa kukosa dawa na chakula. Hayo yanatendeka huku Marekani ikiendelea kufanya sarakasi ya kujenga bandari eti ya kuwafikishia watu wa Gaza misaada ya kibinadamu. Onyesho hilo la kejeli na kichekesho limepoteza kabisa maana mbele ya jinai zinazoongezeka kila siku za Wazayuni dhidi ya Wapalestina wasio na hatia huko Gaza.