Assad: Nitakumbukwa kama muokozi wa uhuru wa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i11245-assad_nitakumbukwa_kama_muokozi_wa_uhuru_wa_syria
Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema kwamba, anataraji kuwa historia itamkumbuka kama kiongozi aliyesimama kidete kutetea uhuru wa kujitawala nchi yake mbele ya chokochoko za mabeberu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2016 11:22 UTC
  • Assad: Nitakumbukwa kama muokozi wa uhuru wa Syria

Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema kwamba, anataraji kuwa historia itamkumbuka kama kiongozi aliyesimama kidete kutetea uhuru wa kujitawala nchi yake mbele ya chokochoko za mabeberu.

Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya NBC, Rais Assad amesema, ana matumaini kuwa madaftari ya historia yatamuandika na kumkumbuka kama kiongozi aliyesimama kutetea na kulinda uhuru wa nchi yake mbele ya uvamizi wa madola ya kibeberu sambamba na kukabiliana na harakati za kigaidi.

Rais wa Syria ameliambia shirika la habari NBC kuwa: "Unaposimama kidete kulinda uhuru wa kujitawala nchi yako, ukabiliane na kisha uangamize magaidi, basi wewe hautahesabiwa kuwa mtu katili, mantiki itahukumu kuwa wewe ni mtetezi na mzalendo halisi."

Aidha Rais wa Syria amekanusha madai kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa Russia na Marekani wamewahi kufanya kikao pamoja naye na kujadili uwezekano wa yeye kuachia madaraka.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu laki nne wameuawa tangu uasi na harakati za kigaidi zinazoungwa mkono na nchi za Magharibi zilikumbe nchi hiyo ya Kiarabu Machi mwaka 2011.