Makumi wauawa shahidi Gaza katika hujuma za anga za Israel
Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zimefanya mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza zikiwemo kambi za wakimbizi na kuua shahidi makumi ya Wapalestina.
Shirika la habari la WAFA limenukuu duru za hospitali zikisema kuwa, watu 10 wakiwemo watoto watatu wameuawa baada ya nyumba zao kushambuliwa kwa mabomu ya utawala wa Kizayuni katika eneo la al-Rumaydah, katika mji wa Khan Yunis, kusini mwa Gaza.
Katika shambulio jingine tofauti la anga mjini Khan Yunis, utawala wa Kizayuni umelenga makazi ya familia ya mwanamuqawama Abu Khater, na kuua shahidi watu wawili na kujeruhi wengine kadhaa.
Kadhalika ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni mapema leo Jumatatu zimeshambulia kambi za wakimbizi za Bureij na Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza na kuua shahidi Wapalestina wengine zaidi ya 10.
Habari zaidi zinasema kuwa, aghalabu ya Wapalestina waliouawa shahidi katika wimbi hilo la mashambulio ya kinyama ya utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza ni watoto wadogo.
Kwa mujibu wa takwimu za karibuni, Wapalestina zaidi ya 36,500 wameuawa shahidi na wengine 82,700 wamejeruhiwa tangu kuanza mauaji ya umati ya utawala wa Kizayun dhidi ya Wapalestina tarehe 7 Oktoba, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.