Jun 27, 2024 07:33 UTC

Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen vimesambaza video inayoonyesha kutumiwa kombora la balestiki la hypersonic dhidi ya meli ya Israeli katika Bahari ya Arabia. Vikosi hivyo vilisambaza video hiyo siku ya Jumatano, vikisema kombora lililotumika linaitwa "Hatem-2" na kwamba meli iliyolengwa ni "MSC SARAH V."

Taarifa inayoambatana na video hiyo inabainisha kuwa kombora hilo limezinduliwa na kutumiwa kwa mara ya kwanza kabisa, na kuwa lililenga shabaha iliyokusudiwa bila kukosea.

Taarifa hiyo imeendelea kuorodhesha baadhi ya sifa muhimu za kombora hilo kuwa ni pamoja na kutumia fueli mango, mfumo erevu wa udhibiti na uwezo wake mkubwa wa kuruka na kukabiliana na hali tofauti katika medani ya vita.

Inasema kombora la "Hatem-2" lina "vizazi kadhaa vyenye masafu tofauti" na kwamba limeundwa na Mamlaka ya Utengenezaji wa Zana za Kijeshi ya Yemeni.

Tangu tarehe 7 Oktoba, wakati utawala wa Israel ulipoanzisha vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza, majeshi ya Yemen yamekuwa yakiendesha operesheni nyingi zikilenga meli za Israel au zile zinazoelekea kwenye bandari za ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.

Kombora la balestiki la hypersonic la Yemen

Vita vya Israel hadi sasa vimegharimu maisha ya Wapalestina zaidi ya 37,700, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, na kujeruhi wengine zaidi ya 86,300.

Vikosi vya Yemen vimeapa kuendeleza mashambulizi yake hayo maadamu utawala wa Israel utaendeleza mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya raia wa Palestina na kudumisha mzingiro wa kidhulma dhidi ya Gaza.

Video ya Jumatano haikuwa ya kwanza kuonyesha vikosi vya Yemen vikizindua silaha na makombora mapya, bali vimekuwa vikifanya hivyo mara kwa mara tangu utawala wa kibaguzi wa Israel uanzishe operesheni ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina mwezi Oktoba uliopita.