Ndege za muungano wa Marekani zaua makumi ya raia nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i11575-ndege_za_muungano_wa_marekani_zaua_makumi_ya_raia_nchini_syria
Kwa akali raia 56 wakiwamo watoto wadogo 11 wamepoteza maisha katika mashambulizi ya anga ya ndege za muungano bandia wa kupambana na magaidi unaoongozwa na Marekani nchini Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 19, 2016 23:01 UTC
  • Ndege za muungano wa Marekani zaua makumi ya raia nchini Syria

Kwa akali raia 56 wakiwamo watoto wadogo 11 wamepoteza maisha katika mashambulizi ya anga ya ndege za muungano bandia wa kupambana na magaidi unaoongozwa na Marekani nchini Syria.

Taarifa iliyotolewa na kundi la watetezi wa haki za binadamu nchini Syria, imesema kuwa shambulizi hilo lilifanywa asubuhi ya jana katika kijiji cha al-Tukhar mkoani Aleppo ambapo makumi ya raia wasio na hatia waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Baadhi ya ripoti nchini Syria zimearifu kuuawa karibu raia 160 katika hujuma hiyo. Rami Abdul Rahman, mkuu wa taasisi hiyo inayojihusisha na masuala ya haki za binadamu na yenye makao yake nchini Uingereza amesema kuwa, kufuatia shambulizi hilo, raia walipatwa na hali ya wasiwasi mkubwa huku wakikimbia huku na huko ili kuokoa maisha yao. Kwa mujibu wa Abdul Rahman, inaonekana hujuma hiyo dhidi ya kijiji cha al Tukhar, kilichopo kilometa 14 kaskazini mwa mji wa Manbij, ilitekelezwa kwa bahati mbaya.

Hadi sasa muungano huo unaoitwa kwa istilahi dhidi ya Daesh haujatoa maelezo yoyote kuhusiana na mauaji hayo ingawa umedai kwamba bado unaandaa ripoti kuhusiana na kadhia hiyo. Hii ni katika hali ambayo kwa akali raia 21 waliripotiwa kuuawa katika shambulizi kama hilo lililofanywa na ndege za muungano huo unaoongozwa na Marekani katika mji wa Manbij mkoani Aleppo, Syria, hujuma iliyotekelezwa siku ya Jumatatu ya wiki hii.

Mji wa Manbij ulidhibitiwa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Desh tangu mwaka 2014, ambapo baadaye uligeuzwa na kuwa ngome kuu ya kundi hilo.