Sheikh Naeem Qasim: Marekani ni mshirika wa jinai za utawala wa Kizayuni
(last modified 2024-09-23T07:09:40+00:00 )
Sep 23, 2024 07:09 UTC

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema Marekani ni mshirika wa mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza na Lebanon.

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la IRIB, Sheikh Naeem Qassem, amebainisha kwa kusema: katika siku za karibuni na kwa uungaji mkono wa Marekani, Israel imefanya jinai tatu za kivita dhidi ya taifa la Lebanon ambazo zimetuumiza sana; na jinai hizi zinadhihirisha unyama na ukatili wa kiwango cha juu kabisa wa utawala wa Kizayuni na hazijawahi kutokea.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amewahutubu Wazayuni akiashiria kwamba uungaji mkono wa Lebanon kwa watu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina utaendelea maadamu vita vya Gaza vingali vinaendelea na akaongeza kuwa: wakaazi wa eneo la kaskazini mwa Palestina linalokaliwa kwa mabavu (Israel) hawatarejea makwao, bali uhamaji wao utaongezeka na uungaji mkono kwa Wapalestina pia utapanuka zaidi.

Siku ya Ijumaa usiku wiki iliyopita  jeshi la Israel lilishambulia eneo la Dahiya kusini mwa Beirut kwa kulenga jengo moja, na kupelekea kuuawa shahidi raia 45 wa Lebanon, akiwemo kamanda wa Jihadi wa Hizbullah Haj Ibrahim Aqil na kujeruhiwa pia makumi mengine ya watu.

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ilitangaza kuuawa kamanda wake wa ngazi ya juu Ibrahim Aqil katika hujuma ya kigaidi iliyotekelezwa Ijumaa na utawala haramu wa Israe jijini Beirut

Utawala huo katili wa Kizayuni pia uliwaua raia wasiopungua 37 wa Lebanon na kuwajeruhi wengine zaidi ya 4,000 katika operesheni za kigaidi za siku ya Jumanne na Jumatano tarehe (Septemba 17 na 18) huko Lebanon kwa kulipua maelfu ya vifaa vya pager, vifaa vya wireless na mifumo ya mawasiliano.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sheikh Naeem Qasim amesisitiza kwa kusema: "tumelenga eneo la Haifa kwa makombora matatu na hii ni sehemu ya kulipiziana kisasi na adui Mzayuni.

Jana Jumapili,  bandari ya Haifa ilifungwa kutokana na mashambulizi makali ya makombora yaHizbollah ya Lebanon  yaliyolenga maeneo mengine ya kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).

Halikadhalika Hizbullah ya Lebanon ilivilenga kwa makumi ya makombora vituo vya kijeshi vya kampuni ya kutengeneza silaha ya Rafael ya utawala wa Kizayuni.

Tags