Hizbullah yaipiga kambi ya kijeshi ya Israel kwa makombora ya Fadi-1
(last modified 2024-09-30T02:27:48+00:00 )
Sep 30, 2024 02:27 UTC
  • Hizbullah yaipiga kambi ya kijeshi ya Israel kwa makombora ya Fadi-1

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imesema imevurumisha makombora ya Fadi-1 dhidi ya kambi ya jeshi la Israel katika maeneo ya kaskazini yanayokaliwa kwa mabavu.

Hizbullah imesema katika taarifa Jumapili kwamba, makombora yake yalilenga kambi ya kijeshi ya Ofek, na kuongeza kuwa shambulio hilo limefanyika kujibu hujuma za Israel dhidi ya ardhi ya Lebanon na raia wa kawaida; sambamba na kuwaunga mkono Wapalestina huko Gaza.

Habari zaidi zinasema kuwa, Hizbullah jana Jumapili pia ilirusha makombora matano kuelekea eneo la Tiberias kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Ving'ora vilisikika katika vitongoji kadhaa haramu vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya kaskazini ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kufuatia mashambulio hayo.

Jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi ya kikatili dhidi ya Lebanon kuanzia Jumatatu ya wiki iliyopita.

Tangu wakati huo, Hizbullah imejibu mapigo kwa wimbi la mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kulenga maeneo ya kijeshi ya Israel na makazi ya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya kaskazini yanayokaliwa kwa mabavu, na vile vile kwenye Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu.

Hizbullah imefanya mashambulio hayo ya kulipiza kisasi baada ya jeshi la Israel kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut na kuua shahidi mamia ya watu na kujeruhi wengine wengi. 

 

Tags