UN: Uhuru wa maoni na kujieleza umekandamizwa vikali katika vita vya Israel dhidi ya Ghaza
(last modified Sun, 20 Oct 2024 02:44:20 GMT )
Oct 20, 2024 02:44 UTC
  • UN: Uhuru wa maoni na kujieleza umekandamizwa vikali katika vita vya Israel dhidi ya Ghaza

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa kuchunguza haki ya uhuru wa kutoa maoni na kujieleza amesema, uhuru wa maoni na kujieleza umehatarishwa vibaya zaidi huko Ghaza kuliko ilivyotokea katika mzozo wowote ule wa hivi karibuni, huku waandishi wa habari wakilengwa katika eneo hilo lenye vita na waungaji mkono wa Palestina wakikandamizwa katika nchi nyingi duniani.

Irene Khan, ambaye ameteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, hakuna mzozo uliotokea katika siku za hivi karibuni ambao umehatarisha uhuru wa kujieleza ndani ya eneo lake na nje ya mipaka yake kama ilivyo katika vita huko Ghaza.

Khan amezungumzia hujuma dhidi ya vyombo vya habari na mauaji ya ulengaji wa makusudi na uwekaji kizuizini kiholela wa makumi ya waandishi wa habari huko Ghaza.

Sambamba na kukosoa hatu ya Israel ya kuvipiga marufuku vyombo vya habari kama Al Jazeera na kuwashambulia waandishi wa habari, mtaalamu huyo wa UN amesema: "hatua hizi zinaonekana kuashiria mkakati wa mamlaka ya Israel kunyamazisha uandishi wa habari muhimu na kuzuia uwekaji kumbukumbu wa uhalifu wa kimataifa ambao yamkini unafanyika."

Vilevile, Khan amekosoa vikali kile alichokiita "ubaguzi na undumilakuwili" unaofanywa wa kuzuia na kukandamiza maandamano na hotuba za kuwaunga mkono Wapalestina.

Ametoa mfano wa marufuku zilizowekwa Ujerumani na katika nchi nyingine za Ulaya, "ukandamizaji mkali" uliofanywa kwenye vyuo vikuu vya Marekani, na namna alama na nembo za kitaifa za Palestina na kauli mbiu za kuwaunga mkono Wapalestina ikiwemo bendera na Kefiyyeh za Palestina zilivyopigwa marufuku na hata kujinaishwa katika baadhi ya nchi.

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa wa kuchunguza haki ya uhuru wa kutoa maoni na kujieleza ametamatisha kwa kueleza kwamba ujumbe wake mkuu ni kuwa kinachotokea Ghaza kinafikisha ujumbe duniani kote kwamba ni sawa kabisa kufanywa mambo hayo kwa sababu yanafanyika Ghaza na Israel inaachwa kikamilifu ifanye itakavyo bila kufuatiliwa kisheria; na hivyo kuwafanya wengine duniani kote waaamini kuwa kutakuwepo uhuru huo kamili wa kufanya uhalifu bila kuwajibishwa".../

Tags