Magaidi wa Daesh waukimbia mji wa Manbij na nguo za kike
Ripoti zinasema kuwa wanamgambo watatu wa kundi la kigaidi la Daesh ambao walitaka kuukimbia mji wa Manbij kaskazini mwa Syria wakiwa wamevalia nguo za kike wamekamatwa mateka na wapiganaji wa Kikurdi.
Wanachama hao watatu wa Daesh walijaribu kuukimbia mji wa Manbij wakiwa wamevalia baibui na kujichanganya na raia wa kawaida sambamba na kumalizika muhula wa masaa 48 uliotolewa na wapiganaji wa Kikurdi wa Syria kwa wapiganaji wa Daesh ili wawe wameondoka huko Manbij.
Vikosi vya Kidemokrasia vya Wakurdi huko Syria vilianzisha oparesheni za kijeshi tarehe 31 mwezi Mei mwaka huu kwa lengo la kuukomboa mji wa Manbij na vikosi hivyo tarehe 3 mwezi Juni mwaka huu vilifanikiwa kuingia katika maeneo ya kusini magharibi mwa Manbij baada ya kuuzingira mji huo.
Magaidi hao wanaoungwa mkono na nchi kama Marekani na Saudi Arabia wamepata pigo kubwa katika siku za hivi karibuni huko Iraq na Syria na sasa wanakimbia ovyo wakiacha nyuma ngome na maeneo waliyokuwa wakiyashikilia kwa miaka kadhaa.