Msalaba Mwekundu: Viwango vyote vya kisheria na kimaadili vimekiukwa huko Gaza
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu amezungumzia hali mbaya ya inayoshuhudiwa sasa katika Ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel na mzingiro mkubwa wa eneo hilo na kusisitiza kuwa, viwango vyote vya kisheria na kimaadili vimekiukwa katika Ukanda wa Gaza.
"Hakuna kinachoweza kuhalalisha kile kinachotokea Gaza," amesema Mirjana Spoljaric, mkuu wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, katika taarifa yake ya hivi karibuni na kuongeza kuwa: "Kiwango cha mateso ya binadamu na kukanyagwa utu wao vinazidi viwango vyote vinavyokubalika vya kisheria na kimaadili."
Amesema, "kila dakika inayopita bila kusitishwa mapigano ina maana ya kuaga dunia raia wengi zaidi. Kiwango cha mateso ya raia kinachosababishwa na vita visivyobagua na kunyimwa mahitaji ya kimsingi ya maisha ni cha kutisha."
Mirjana Spoljaric amesema: "Kifo kinawanyemelea raia wanaotafuta chakula, watoto wanakufa kwa kukosa chakula, na familia zinalazimika kukimbia tena na tena kutafuta usalama ambako haupo."
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu amesisitiza kuwa: "Maafa haya lazima yasitishwe mara moja. Kusitasita kokote kisiasa na jaribio lolote la kuhalalisha jinai zinazofanywa mbele ya macho ya walimwengu ni kielelezo cha kushindwa kwa pamoja kwa dhamiri ya walimwengu kuhusiana na kudumisha kiwango cha chini kabisa cha ubinadamu katikati ya vita."
Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza ilitangaza siku ya Ijumaa kwamba idadi ya Wapalestina waliouawa na jeshi la Israel hadi sasa inakaribia watu elfu 60.