Hamas: Israel imeingia katika marhala mpya ya mauaji ya kimbari Gaza
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imelaani vikali mpango wa Israel wa kukalia kwa mabavu Jiji la Gaza na kuwahamisha kwa nguvu wakazi wake na kusisitiza kuwa, huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Hamas ilisema hayo katika taarifa iliyotumwa kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Telegram jana Jumapili, kufuatia uamuzi wa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuchukua udhibiti kamili wa Gaza City, mji mkubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza na kuonya kwamba, hatua hiyo inaashiria kuanza awamu mpya ya mauaji ya halaiki na kulazimishwa kuhama mamia ya maelfu ya watu katika eneo hilo.
"Mipango ya kuikalia Gaza na kuwafurusha wakazi wake ni uhalifu mkubwa wa kivita ambao unaonyesha kutozingatia utawala huo ghasibu sheria za kimataifa na za kibinadamu," imesema Hamas.
Kadhalika Hamas imetilia shaka mazungumzo ya Israel ya eti kujenga makazi na kuwapa usaidizi wa kibinadamu wakazi wa kusini mwa Ukanda wa Gaza, ikiitaja hatua hiyo kama mbinu ya hadaa na udanganyifu, ili kuficha mpango wake wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Gaza.
Kundi hilo la Muqawama pia limesema kwamba, uungaji mkono wa kisiasa na kijeshi wa Marekani umeushajiisha utawala huo kuendelea na vitendo vyake vya mauaji ya kimbari na kufuta kizazi.
Wakati huo huo, Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imelaani uamuzi wa jeshi la Israel wa kusambaza mahema kusini mwa Gaza, na kuuleza kama sehemu ya mpango wa utawala huo pandikizi wa kuwahamisha kwa nguvu wakazi wa Jiji la Gaza kutoka kaskazini hadi kusini na kuuteka mji huo.