Feb 16, 2016 01:06 UTC
  • Bahrain inakiuka haki za watoto wadogo

Utawala wa Aal Khalifa unaendelea kukiuka haki za binadamu hususan za watoto wadogo wa nchi hiyo.

Gazeti la al Akhabari limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa utawala wa Bahrain unaendelea kuwatia mbaroni na kuwatesa raia wa nchi hiyo hususan watoto wadogo kwa kisingizio kuwa ni magaidi, licha ya vitendo hivyo kulaaniwa kimataifa na licha ya kuwa vinapingana na hati ya kimataifa iliyoidhinishwa na Bahrain yenyewe kuhusu haki za watoto.

Gazeti hilo limeongeza kuwa, kwa mujibu wa takwimu na taarifa za Taasisi ya Sheria ya Bahrain, zaidi ya watoto 250 wamefungwa katika jela mbalimbali za nchi hiyo. Wengi wa watoto hao wametiwa nguvuni kwa sababu za kisiasa na baadhi yao wanasubiri kuhukumiwa kwa sheria eti za kupambana na ugaidi.

Kituo cha Haki za Binadamu cha Bahrain kimetangaza kuwa mwezi Novemba mwaka jana, idadi kubwa ya watu waliotiwa mbaroni walikuwa watoto ambao idadi yao imetajwa kufikia 100.

Hii ni katika hali ambayo taasisi 9 za binadamu tarehe 20 mwezi Novemba mwaka jana zilitoa taarifa ya pamoja zikieleza kuwa maafisa wa Bahrain tangu mwaka 2011 hadi hivi sasa wameshauwa watoto zaidi ya kumi na hivyo kukiuka haki za watoto na wanaendelea kuwashikilia korokoroni watoto wengine zaidi 1,015 chini ya sheria ya eti kupambana na ugaidi.

Tags