Jeshi la Iraq limeangamiza Madaesh 700 katika kisiwa cha Khalidiya
Jeshi la Iraq limetangaza kuwa limefanikiwa kuangamiza mamia ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika operesheni ya kukomboa kisiwa cha Khalidiya, kilichopo mashariki mwa mji wa Ramadi, magharibi mwa mkoa wa Anbar.
Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Meja Jenerali Ismail Mahalawi, kamanda wa operesheni za Anbar na kuongeza kuwa, kufikia sasa jeshi la Iraq limefanikiwa kuangamiza wanachama 700 wa kundi la Daesh tangu operesheni ya kukisafisha kisiwa hicho cha kistratajia ilipoanza, baada ya kukombolewa kwake wiki mbili zilizopita.
Mapema mwezi huu wa Agosti, vyombo vya habari nchini Iraq vilitangaza habari za kukombolewa kisiwa hicho toka mikononi mwa matakfiri wa Daesh, kisiwa ambacho kimekuwa mikononi mwa matakfiri hao tangu wauteke mji wa Ramadi mwezi Mei mwaka 2014.
Inafaa kukumbusha kuwa, jeshi la Iraq kwa kushirikiana na harakati za kujitolea za wananchi, lilianzisha operesheni ya kuukomboa mji wa Ramadi, kati ya Disemba mwaka uliopita na Februari mwaka huu.
Hii ni katika hali ambayo, Ibrahim al-Awsaj, meya wa mji wa Ramadi hivi karibuni alisema kufuatia kurejea hali ya usalama kwa kipindi cha miezi saba iliyopita kwenye maeneo ya mkoa wa Anbar, maelfu ya familia zilizolazimika kuyakimbia maeneo hayo katika muda ambao wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh walipoyadhibiti, sasa zimereja makwao.