Sayyid Hassan Nasrullah: Hizbullah itaishinda Israel katika vita vyovyote vipya
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema: endapo vitaanzishwa vita vyovyote vipya dhidi ya Lebanon, Hizbullah itaibuka mshindi katika medani hiyo.
Sayyid Hassan Nasrullah ameyaeleza hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Manar na kubainisha kuwa ushindi wa Muqawama katika vita vya siku 33 vya mwaka 2006 halikuwa tukio la kawaida, hali ya kuwa mashambulio yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni katika vita hivyo yalikuwa makubwa zaidi kuliko ilivyokuwa katika vita vyote baina ya utawala huo na nchi za Kiarabu; na mashambulio yote hayo yalifanywa kwa uungaji mkono wa kimataifa na kieneo na kwa lengo moja tu ambalo lilikuwa ni kuuangamiza muqawama.
Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kwa kusema:"endapo vitaanzishwa vita vipya dhidi ya Lebanon tungali na uhakika kuwa muqawama utashinda."
Ameongeza kuwa: miongoni mwa masuala muhimu uliyokiri utawala wa Kizayuni ni kwamba kama sisi tunataka kuishinda Hizbullah jambo hili halitowezekana kupitia vita na makabiliano ya ana kwa ana; na kupigana vita na Iran pia hakuna faida na ndio maana wamedhamiria kuitoa Syria nje ya mhimili wa muqawama.
Sayyid Hassan Nasrullah ameongeza kuwa lengo kuu la vita vya siku 33 lilikuwa ni kuutokomeza muqawama Lebanon, Syria na Palestina na hatimaye kuitenga Iran.
Katibu Mkuu wa Hizbullah amebainisha kuwa tatizo walilonalo maadui wa Syria na Rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad ni kwamba yeye hayuko tayari kuikubali Mashariki ya Kati Mpya yenye maana ya kuweko madarakani watawala na viongozi watakaosalimu amri kwa Marekani.
Katika sehemu nyengine ya mahojiano hayo na kanali ya televisheni ya al-Manar, Nasrullah amesema nchi za Kiarabu na makundi ya kitakfiri yanafanya kazi ya kuuhami na kuusaidia utawala wa Kizayuni.../