Pakistan yakataa wito wa Marekani wa kuanzisha uhusiano na 'Israel'
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i138660-pakistan_yakataa_wito_wa_marekani_wa_kuanzisha_uhusiano_na_'israel'
Pakistan imekataa wito wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa kuitaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, Khawaja Asif, amesema pendekezo hilo kuwa “halikubaliki” na linakwenda kinyume na misingi ya taifa hilo.
(last modified 2026-05-27T03:14:39+00:00 )
May 27, 2026 03:12 UTC
  • Khawaja Asif
    Khawaja Asif

Pakistan imekataa wito wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa kuitaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, Khawaja Asif, amesema pendekezo hilo kuwa “halikubaliki” na linakwenda kinyume na misingi ya taifa hilo.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Pakistan, Samaa TV, Asif amesema Islamabad haiwezi kuunga mkono makubaliano yanayokinzana na “itikadi za msingi” za nchi hiyo.

Kauli hizo zilijiri baada ya kuulizwa kuhusu uwezekano wa Pakistan kujiunga na kile kinachoitwa 'Mapatano ya Abraham', ambayo ni makubaliano yaliyoratibiwa na Marekani yaliyosababisha baadhi ya mataifa ya Kiislamu kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel. Rais Trump anashinikiza nchi nyingi za Kiislamu zijiunge na mapatano hayo.

Akihoji uaminifu wa utawala wa Kizayuuni wa Israel, Asif alisema: “Unawezaje kukaa meza moja na watu ambao huwezi kuamini neno lao hata kwa siku moja?”

Waziri huyo pia amesisitiza msimamo wa muda mrefu wa Pakistan kuhusu suala hilo. “Tuna msimamo ulio wazi kabisa kwamba jambo hili halikubaliki kwetu."

Akirejelea sera ya pasi za kusafiria za Pakistan, Asif ameongeza kuwa Pakistan ndiyo nchi pekee ambayo pasi zake za kusafiria “hazitambui hata jina la Israel.”

Kauli hizo zimekuja wakati Trump akiendelea kushinikiza mataifa zaidi kufuata nyayo za Umoja wa Falme za Kiarabu,  Bahrain, na Morocco ambazo tayari zimeingia katika makubaliano ya kuwa na uhusiano na utawala haramu wa Israel chini ya 'Mapatano ya Abraham'.

Trump amesema mataifa kama Saudi Arabia na Qatar yanapaswa kujiunga “mara moja” na makubaliano hayo kabla ya kufikiwa kwa makubaliano yoyote kati ya Iran na Marekani kuhusu kusitisha kikamilifu vita dhidi ya Iran.

Wapalestina pamoja na waungaji mkono wao wameendelea kulaani kwa sauti kubwa makubaliano hayo, wakizishutumu nchi za eneo zilizoyatia saini kuwa kuwa zimesaliti harakati za kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel.